AKILI ZA KIJIWENI: Tumeshtukia wajanja dili la Sowah

YULE Jonathan Sowah ni ingizo muhimu sana kwa Singida Black Stars katika dirisha dogo lililopita kutokana na kasi yake ya kufumania nyavu akimfunika hadi straika aliyemkuta Elvis Rupia.

Namba hazidanganyi bhana kwani Sowah katika mechi saba alizocheza ameshafunga mabao saba kwamba ana wastani wa bao moja katika kila mchezo wa Ligi Kuu Bara sasa kupinga hata hizo takwimu itakuwa ni kichekesho.

Na kinachombeba zaidi Mghana yule ni kwamba amekuwa ni mpigaji mzuri wa penalti kama Lionel Ateba wa Simba hivyo tuta linapotokea wala hawajishauri ngoma inaanguka kwa Sowah.

Siku moja hapa kijiweni zikavuma tetesi kwamba wale jamaa wa kijani pale katika kata ya Jangwani wanammiliki kimyakimya mchezaji huyo wa zamani wa Medeama na pale Singida Black Stars kawekwa kama aangaliwe tu kama vitu vimo au havimo.

Hili sio suala la kushangaza maana ile timu na Singida Black Stars ni klabu rafiki na ndio maana siku zote wanapeana tu wachezaji kirahisi au hata makocha bila hata kudaiana mapesa kwa sababu ya kulinda urafiki wao ambao sababu kila mmoja anaijua tusisumbuane maana wote tumesoma Cuba.

Na jamaa siku moja alihojiwa akasema kiongozi wa ile timu ni kama baba yake na anamheshimu sana kwa vile amemsaidia sana katika maisha yake kabla hata hajaja Tanzania kucheza soka la kulipwa hivyo ni wazi kwamba imeshaanza kujulikana wapi Sowah ataenda baada ya msimu kumalizika.

Sasa kuna wajanja au watu wa kati hao wameamua kutaka kujifanya wao wana akili nyingi kuliko wengine wakatengeneza mchongo kwamba timu nyingine kubwa inayovaa jezi nyekundu na nyeupe inamtaka Sowah na inajipanga kwenda kuzungumza na Singida Black Stars ili iwauzie.

Hakuna kitu kama hicho kiuhalisia, lakini wanajaribu kumpandisha thamani Sowah ili ule upande ambao una uhakika wa kumchukua, ulazimike kutoa pesa nyingi kumpata ili nao waweze kupiga cha juu tofauti na ilivyo sasa ambapo watapata kidogo au hawatopata kabisa.

Hao ndio watu wa kati wa usajili, wamekaa kidilidili sana na hawaoni woga wa kutengeneza mchongo bandia wa usajili ili jambo lao tu lifanikiwe.

Related Posts