Mwanza. “Tunakosa vingi sana.” Ndivyo anavyoanza kusema mkazi wa Tarime mkoani Mara, Christopher Sereri (52) akieleleza magumu anayopitia kutokana na mapengo aliyoyapata baada ya kung’oa meno sita kwenye.
Sereri ambaye amesumbuliwa na meno kwa zaidi ya miaka 21 iliyopita anasema kutokana na kusumbuliwa na tatizo la kutoboka meno alilazimika kung’oa, huku akilalamika kukosa vinono kutokana na changamoto hiyo.
Kutokana na kung’olewa meno hayo, Sereri ana mapengo sita kwenye taya zote mbili jambo ambalo anadai limebadili kabisa mwonekano wa uso wake kutokana na kuonekana umepinda na kubonyea.
Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Machi 20,2025, wakati wa shughuli ya upimaji wa afya ya kinywa bila malipo kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa iliyofanyika Bugando Mwanza, Sereri amelalamika kukosa vinono, kwani mapengo hayo yanamkwamisha kula baadhi ya vyakula vigumu ikiwemo nyama, mahindi ya kuchoma na mihogo anavyodai hutamani kuvila ila sasa anaishia ‘kula kwa macho.’
“Mbali na kukosa vinono, kuna wakati nakosa kujiamini kwa sababu kwenye jamii naogopa hata kucheka. Wengine wakiniangalia wananicheka. Napitia wakati mgumu sana,” amesema Sereri.
Simulizi ya Sereri haitofautiani na ile ya Mkazi wa Mtaa wa Miembeni Kata Pamba jijini Mwanza, Johari Rashid (53) ambaye naye ana mapengo yaliyotokana na kung’olewa meno sita.

Mkuu wa Idara ya Kinywa na Meno ambaye ni Daktari Bingwa Mpangilio wa Meno katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dk Alex Elius alitoa elimu ya Afya ya kinywa na Meno kwa wakazi wa kanda ya Ziwa wakati wa maadhimisho ya siku ya Kinywa na Meno yaliyofanyika Kikanda Hospitali ya Bugando jijini Mwanza. Picha na Mgongo Kaitira
“Jamii inanicheka, kuna baadhi ya vyakula ninashindwa kuvila.”
Johari ambaye ni mjane anasema matamanio yake ni kuwekewa meno ya bandia japo ‘ukata’ ni kikwazo kingine kinachokwamisha ndoto hiyo kutimia, kwa kile alichodai kupandikiza meno ya bandia ni gharama asiyoweza kuimudu.
“Ninatamani sana kuwekewa meno ili angalau nifurahie baadhi ya vyakula, lakini sasa angalia mdomoni ulivyo. Watu wakiniona nazungumza ama nacheka wananicheka,” amesema Johari.
Mkuu wa Idara ya Kinywa na Meno ambaye ni Daktari Bingwa Mpangilio wa Meno katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Dk Alex Elius amesema kuna sababu lukuki zinazosababisha mgonjwa kulazimika kung’olewa jino lake.
Dk Elius ametaja sababu hizo kuwa ni pamoja na jino kutoboka, ajali, uvimbe kwenye taya na meno husika sambamba na sababu zisizoweza kuzuilika pindi mgonjwa anapopata changamoto.
Amesema Idara ya Kinywa na Meno Bugando inahudumia wastani wa wagonjwa 1,000 kwa mwezi kati yao zaidi ya 760 sawa na asilimia 76.5 wakisumbuliwa na tatizo la jino kutoboka ikifuatiwa na uvimbe kwenye fizi.
Pia, amesema wastani wa wagonjwa 24 wanafanyiwa upasuaji mkubwa ukiwemo wa kuondoa uvimbe, meno yaliyooza, fizi zilizovimba, saratani na mpangilio mbaya wa meno kila mwezi.
Dk Elius ametaja sababu za meno kuharibika kuwa ni pamoja na kutopiga mswaki ipasavyo na angalau mara mbili kwa siku, kwa kutumia dawa ya meno iliyotengenezwa kwa madini ya Flouride.
Pia, ametaja mtindo mbaya wa maisha hususan ulaji holela wa vyakula vyenye sukari nyingi, kutokula mlo kamili, kutokunywa maji ya kutosha, kukaa na changamoto za kiafya kwa muda mrefu na kutofanya uchunguzi mara kwa mara.
“Watu wanapiga mswaki ila hawapigi inavyohitajika. Tunapaswa kufuata ushauri wa wataalamu wa kinywa ikiwemo kupiga mswaki si chini ya dakika tatu. Na uhakikishe kuwa kila jino umeligusa kulisafisha kwa kutumia dawa ya meno,” amesema Dk Elius.
Madhara ya mapengo kitaalamu
Dk Elius ametaja adha ya kuwa na mapengo kitaalamu kuwa ni pamoja na kuharibu mpangilio wa meno.
“Meno yana tabia ya kuziba eneo lililo wazi hivyo kuhamisha taya za muhusika na kusababisha sura au meno kukaa katika mpangilio usiovutia.”
Pia, amesema ina athari kwenye mmeng’enyo wa chakula. “Baadhi ya vyakula hususan vyenye ‘wanga’ ambavyo mmeng’enyo wake huanzia mdomoni hakitochakatwa ipasavyo hivyo kuathiri afya ya muhusika.
Amesema mapengo pia husababisha changamoto ya kisaikolojia kutokana na muhusika kukumbana na unyanyapaa kwenye jamii. Pia, huathiri muundo wa mwili kiasi cha kuathiri namna ya ubongo kuchakata shughuli za kimwili.
Ukeketaji viungo vya kinywa
Awali, akizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando, Dk Bahati Wajanga, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Bugando, Dk Alicia Masenga amesema miongoni mwa changamoto zinazoitesa Kanda ya Ziwa ni mila na desturi potofu ikiwemo ya kukeketa viungo vilivyoko kwenye kinywa.
Dk Masenga ametaja baadhi ya viungo vinavyokeketwa na kuondolewa ni pamoja na ‘kimeo’, na kinachoitwa meno ya nyoka ambayo vichanga hung’olewa kwa nguvu kwa kisingizio kuwa huwasababishia homa.
Pia imani potofu ya kuwa wajawazito hawatakiwi kutibiwa meno.
“Tumekuwa tukiletewa wajawazito wanaoumwa meno ambayo yamefikia hatua mbaya wakati mwingine uvimbe ambao umegeuka kuwa sararani. Pia, kuna watoto ambao wanang’olewa meno katika jamii bila kuzingatia ushauri wa kitaalamu,” amesema Dk Masenga.
Dk Masenga ameitaka jamii hususan ya Kanda ya Ziwa kuachana na mila na desturi hizo zilizopitwa na wakati badala yake wawapeleke wagonjwa hospitalini kupatiwa matibabu ya kitaalamu.
Pia, amesema Bugando imeanza maandalizi ya kuanzisha Kitengo Kikubwa cha Matibabu ya Afya ya Kinywa na Meno kitakachohudumia Kanda ya Ziwa na Magharibi ili kuimarisha huduma hiyo.