Morogoro. Dereva anayetuhumiwa kutaka kulichoma moto lori baada ya kuiba mafuta yenye thamani ya Sh77.1 milioni, amekamatwa na polisi.
Dereva huyo mkazi wa Tabata Kinyerezi jijini Dar es Salaam, Abubakar Mwichangwe (29) amekamatwa kwa tuhuma za kula njama ya kuharibu lori la mafuta na tela lake kwa kulichoma moto, tukio lililotokea usiku wa Machi 16 mwaka huu, akiwa kwenye lori aina ya FAO kampuni ya Meru akitokea Dar es Salaam kuelekea Lubumbashi nchini DR Congo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 20, 2025 mkoani hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema dereva huyo amekamatwa katika mji mdogo wa Chalinze Mkoa wa Pwani baada ya kutafutwa kwa siku kadhaa kufuatia tukio hilo Machi 16 mwaka huu eneo la Msimba Mikumi.
Kamanda Mkama amesema gari hilo lilibeba mafuta aina ya dizeli lita 35,700 yenye thamani ya Sh77.1 milioni mali ya kampuni ya Acer Logistics (T) yalikuwa yakisafirishwa kwenda nchi ya DR Congo.
“Tunawashikilia watu 12 kwa tuhuma mbalimbali akiwemo dereva wa lori la mafuta na mkazi wa Tabata Kinyerezi jijini Dar es Salaam, Abubakar Mwichangwe (29) tuliyemkamata eneo la Chalinze Mkoa wa Pwani kwa tuhuma za kula njama ya kuharibu kwa kulichoma moto gari kwa lengo la kufuta ushahidi baada ya kuiba mafuta aina ya dizeli yenye thamani ya Sh77.1 milioni Machi 16 mwaka huu eneo la Msimba Mikumi mkoani Morogoro,” amesema Kamanda Mkama.
Juzi, Kamanda Mkama alisema baada ya mafuta kuibwa dereva huyo aliwasha moto akijaribu kuliteketeza gari hilo ambapo kabla ya moto huo haujashika walitokea wasamaria wema na kufanikiwa kuuzima moto huo na kutoa taarifa Polisi.
Kwa mujibu wa Kamanda Mkama watuhumiwa watatu wanaotuhumiwa kula njama na dereva huyo walikamatwa.

Waliokamatwa ni Hamidu Sudi (50) mkazi wa Dar es Salaam, Abiner Shalon (25) mkazi wa Morogoro na Abdalah Nihed (30) mkazi wa Morogoro ambao wote ni mameneja wa vituo vitatu vya mafuta vya kampuni ya Simba Oil vilivyopo mkoani humo.
Kwa upande wake mmoja wa wasimamizi wa Simba Oil, Alif Mbaraka, alikiri kufungwa kwa vituo vya kampuni hiyo tangu Machi 16 na kukamatwa kwa mameneja wawili, mmoja kutoka Mjini Kati na mwingine Mkambarani.
Wakati huohuo Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linawashikilia watu 10 kwa tuhuma za kufanya ujangili katika hifadhi iliyo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa).
Kukamatwa kwa watu hao kunatokana na askari wa kikosi maalumu cha Jeshi la Polisi na askari wa hifadhi za Taifa za wanyamapori na kukutwa na silaha za moto na asili zinazodaiwa kutumika katika uwindaji haramu wa wanyamapori.
Kamanda Mkama amesema watuhumiwa hao wamekamatwa Machi 14 mwaka huu baada ya msako uliofanyika vijiji vinavyopakana na hifadhi ya Mikumi wakiwa na bunduki mbili aina ya ‘short gun’ na gobole moja inayotumia risasi za ‘short gun’.
Kamanda Mkama amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Safari Tamba (23) mkazi wa Tanga, Jacob Chigange (50) mkazi wa Melela, Marthias Ndalu (20) mkazi wa Melela, Hussein Rashid (66), Athuman Matonya (48) mkazi wa Vianzi Mlandizi, Ismail Mahyoro (75) mkazi wa Tandika Dar es Salaam, Shabaan Kalesela (50) na Bakari Nzile (53) wakazi wa Mkundi.
Wengine ni Abdulllkarim Mashaka (55) mkazi wa Kilombero na Nestory Mkami (58) mkazi wa Melela Mlandizi.
Kamanda Mkama ametaja silaha nyingine kuwa ni risasi 22, vichwa sita vya risasi za kienyeji, maganda tisa ya ‘short gun’, vifaa vya kutengenezea risasi, risasi 139, na baruti kopo mbili ndogo huku wakiwa wamekamatwa na vichwa viwili vya mnyama aina ya Nsya, miiba 128 ya mnyama nungunungu, upinde mmoja, mishale minne na vichwa vya mishale 15.