Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa chama cha NLD, Hassan Doyo amechukua fomu ndani ya chama hicho kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwania urais wa Tanzania, huku akieleza sababu ya kutaka nafasi hiyo, akibainisha vipaumbele kumi.
Doyo amesema vipaumbele hivyo atavitumia iwapo chama hicho kitampitisha kuwania urais kuvinadi kwa wananchi ambao nao wakimpa ridhaa ya kuwaongoza atavitekeleza.
Katibu mkuu huyo anajitosa ndani ya chama hicho kuungana na vyama vingine vinne, ambavyo navyo harakati za kuwapata wagombea zinaendelea ili kwenda kuchuana Oktoba 2025 kwenye uchaguzi huo,
Mbali na Doyo, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu naye ameonesha nia ya kuwania urais, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ADC Bara, Innocent Siriwa naye ameonesha nia ndani ya chama chake.
Wote hao Semu na Siriwa wamebainisha vipaumbele vyao na kusubiri michakato ya ndani ya vyama vyao kumpata mgombea mmoja.

Aidha, Chama cha Mapinduzi (CCM) chenyewe tayari kimekwisha kuwateua Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wake na Dk Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza.
Leo Alhamisi, Machi 20, 2025, katika ofisi za makao makuu ya NLD Tandika jijini Dar es Salaam, Doyo akiwa na baadhi ya wanachama na viongozi wamejitosa kuchukua fomu, huku akimpongeza Rais Samia kwa kazi nzuri anazozifanya.
Baada ya kiongozi huyo kukabidhiwa fomu amesema kipaumbele chake cha kwanza ni kuhakikisha Watanzania wanapata ajira tatizo ambalo limedumu nchini kwa muda mrefu.
“Jambo la pili ni elimu, tutahakikisha elimu tunayotoa si ya kuhudhuria darasani bali itakuwa elimu yenye manufaa kwa wananchi, ni jambo la ajabu kumwambia muhitimu wa chuo kikuu arudi kujifunza masuala ya ufundi, sisi tutawafanya wahitimu waingie sokoni moja kwa moja,” amesema.
Mbali na hayo, kilimo na ufugaji ni eneo lingine alilotangaza Doyo serikali yake itaipa kipaumbele kwani sasa uwekezaji unaofanyika kwenye sekta hizo ni hafifu.
“Tutaifanya kilimo kiwe cha tija, mchele utauzwa Sh1,000 kwa kilogramu moja, uzalishaji utakuwa mkubwa, kwa upande wa mifugo tutatumia ipasavyo bidhaa za ngozi kutajirisha Watanzania,” amesema.
Pia, Doyo katika kipaumbele chake kingine amesema rasilimali ya mali ambayo itatumika kukuza pato la taifa na kufuta utegemezi wa Tanzania nje ya nchi.
Kupambana na rushwa na ukwepaji kodi nayo Doyo amesema ameyapa kipaumbele akisema zipo ripoti mbalimbali zinazoonyesha kiwango cha rushwa nchini lakini, hakuna hatua madhubuti za kukomesha wala rushwa.
“Tutajenga taifa la walipakodi, walipakodi nchini ni wachache Serikali yangu itakuwa na mazingira rafiki ya ulipaji kodi, nitashusha kodi ya ongezeko la thamani VAT kutoka asilimia 18 hadi 10 ili kila mtu alipe,” amesema.
Kipaumbele kingine alichotaja Doyo ni kuongeza mwamko wa wanawake katika elimu hususan teknolojia akisema kundi hilo ni dogo kwenye masuala ya teknolojia.
Mbali na hayo amesema atahakikisha anaimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kuondoa mambo yanayoonekana kero za muungano huo.
“Tutaimarisha sekta binafsi, sekta binafsi ndio inayoboresha Serikali kwa kuondoa changamoto za wananchi ikiwemo suala la ajira, pia tutaboresha sekta ya madini tunufaike nazo kwa kiwango kikubwa,” amesema.

Akizungumzia vipaumbele hivyo Mchambuzi wa masuala ya siasa, Samson Sombi amesema vipaumbele siku zote havipitwi na wakati tatizo ni kuvitekeleza.
“Kwa mazingira ya Tanzania vipaumbele hivyo havijapitwa na wakati, wanasiasa wengi wanatoa vipaumbele lakini wanakwama kuvitekeleza kwa sababu wanavyovitoa ni vya kisiasa,” amesema.