Tabora. Mkazi wa Mtaa wa Malagarasi mkoani Tabora, Christina Nashon (15) amekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kuiba na kutoroka na mtoto wa mwajiri wake, Beatrice Kiboma mwenye umri wa miezi mitatu na wiki moja.
Christina aliyekuwa anafanya kazi katika familia ya Beatrice yenye makazi yake Kata ya Cheyo Manispaa ya Tabora mkoani humo, anadaiwa kutoroka na kichanga hicho chenye umri wa miezi mitatu na wiki moja Machi 19, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Machi 20, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema binti huyo amekamatwa na wananchi kwa ushirikiano na jeshi hilo, ambapo alikua akitoroka na mtoto huyo kuelekea nyumbani kwao mkoani Kigoma.
Kamanda Abwao amesema mtuhumiwa alifika Tabora Machi 18, 2025 akiwa ameongozana na rafiki yake, Coladula Deo kwa lengo la kufanya kazi za ndani na baada ya kupata kazi hiyo, aliona kazi za kufanya ni nyingi kwa mwajiri wake ndipo alipoamua kutoroka na mtoto huyo.
“Taarifa za awali zinaonyesha kuwa kutoroka kurudi kwao na mtoto huyo kwani wakati anaondoka kwao alidanganya kuwa ana ujauzito, hivyo amelazimika kuondoka na mtoto ili akamuonyeshe nyumbani kwao,” amesema Abwao.

Kamanda wa polisi mkoa wa Tabora, Richard Abwao akizungumza na waandishi wa habari hilo ofisini kwake leo Machi 20, 2025. Picha na Hawa Kimwaga.
Abwao amesema kupitia mahojiano na binti huyo, wamebaini kuwa alikua akifanya mawasiliano na mama yake akimueleza kuwa ameshajifungua hivyo anarudi nyumbani na mtoto wake, na ndio sababu ya kutoroka na mtoto huyo.
Kamanda Abwao amesema jeshi hilo linaendelea kumshikilia ‘Hausigeli’ huyo na rafiki yake kwa mahojiano zaidi na uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani.
Akizungumzia tukio hilo, mama mzazi wa mtoto, Daniela Dotto amesema ‘Hausigeli’ huyo alimdanganya kuwa anaenda nje kuanika nguo za mtoto kisha kutokomea kusikojulikana.
“Alisema anaenda kuanika nguo lakini baada ya muda alitoweka na mtoto mimi nimetoka ndani baada ya kuona kengele ya kuchezea mtoto hailii tena ndio nikatoka nje kufuatilia,” amesema Daniela.
Naye, Baba mzazi wa mtoto huyo, Dotto Mwalembe amesema alipigiwa simu na mke wake kumpa taarifa ya kupotea kwa mtoto, hivyo aliwahi Kituo cha Polisi kutoa taarifa na kutokana na tayari zilikuwa zimeshasambaa zilisaidia kumpata binti huyo akiwa na mtoto wao.
“Tulimkuta akitoa fedha kwa wakala kabla ya kuingia kituo cha mabasi ili aondoke na mtoto wetu. Nawashukuru sana Polisi na jamii kwa kusaidia kumpata mtoto wetu,” amesema Mwalembe.