Dar es Salaam. Kumekucha. Joto la urais wa Tanzania na Zanzibar limeanza kupanda katika baadhi ya vyama vya siasa kwa baadhi ya makada kutangaza nia au kuchukua fomu ya kuomba uteuzi wa kuwania nafasi hiyo ya juu.
Tayari baadhi ya waliotangaza nia ya kuutaka urais kupitia vyama vyao, wameshaweka wazi vipaumbele vyao endapo watapewa ridhaa ya kushika dola.
Hata hivyo, inaonekana mapema kwa baadhi ya vyama kuanza mchakato sasa, jambo ambalo wasomi wanasema ni uamuzi mzuri unaoweza kuwasaidia kwa unatoa nafasi kubwa kwa wanachama kuwajua na hata vyama kujiandaa kwa hatua zijazo.
Uchaguzi Mkuu Rais wabunge na madiwani, unatarajiwa kufanyika Oktoba 2025 na utasimamiwa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).
Wakati hali ikiwa hivyo kwa vyama vingine, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeendelea kukaza uzi na ajenda yake ya No Reforms No Election kikitarajia keshokutwa kuanza mikutano ya kuelimisha umma nchi nzima.
Kwa upande wa Chama cha Mapinduzi (CCM), kilishamaliza mchakato wake, baada ya kuwateua wagombea wake wa nafasi hiyo kwa Jamhuri na Zanzibar, Januari 19, 2025.
Wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipitishwa kuwania tena urais wa Muungano, Dk Hussein Mwinyi alipitishwa na CCM urais wa Zanzibar.
Hukohuko Zanzibara, mwingine aliyetangaza nia ni Othman Masoud Otkman, mwenyekiti wa ACT-Wazalendo anayesubiri mchakato wa chama hicho.
Mbali na Rais Samia aliyepitishwa na CCM, mwingine aliyetangaza ni hiyo ni Dorothy Semu, Kiongozi wa ACT Wazalendo ambaye ametangaza nia ya kuomba ridhaa ya chama hicho kuwania urais wa Tanzania.
Sambamba na hao, Hassan Doyo amechukua fomu ya kuomba kuwania urais kwa tiketi ya NLD huku Innocent Siriwa, naibu katibu mkuu wa Chama cha ADC Bara, akitangaza nia ya kuomba nafasi hiyo ndani ya chama chake.
Wakati makada wanaendelea kujipima na kujitokeza, Chama cha Ada-Tadea kimetangaza kutoa fomu bure kwa wagombea wa makundi maalumu kwa nafasi zote.
Leo Alhamisi, Machi 20, 2025, Doyo amechukua fomu ndani ya chama ya NLD akibainisha vipaumbele kumi, mojawapo kikiwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata ajira.
Jambo la pili ni elimu, akilenga kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa yenye manufaa kwa wananchi.
“Ni jambo la ajabu kumwambia muhitimu wa chuo kikuu arudi kujifunza masuala ya ufundi, sisi tutawafanya wahitimu waingie sokoni moja kwa moja,” amesema.
Mbali na hayo, kilimo na ufugaji ni eneo lingine alilotangaza Doyo, kuwa Serikali yake itaipa kipaumbele kwa kuwa uwekezaji unaofanyika kwenye sekta hizo ni hafifu.
“Tutakifanya kilimo kiwe cha tija, mchele utauzwa Sh1,000 kwa kilo, uzalishaji utakuwa mkubwa, kwa upande wa mifugo tutatumia ipasavyo bidhaa za ngozi kutajirisha Watanzania,” amesema.
Pia, Doyo amesema atapambana na rushwa na ukwepaji kodi na kujenga taifa la walipakodi huku akishusha kodi ya ongezeko la thamani kutoka asilimia 18 hadi asilimia 10 ili kila mtu alipe.
Vipaumbele vingine ni kuongeza mwamko wa wanawake katika elimu ya teknolojia, kuimarisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuipa nafasi sekta binafsi.
Alipotangaza nia ya kugombea Januari 16, 2025, Semu alitaja mambo manne yaliyomsukuma kuitaka nafasi hiyo.
Mambo hayo ni kushuka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, kupanda kwa gharama za maisha, changamoto za ajira kwa vijana na udhaifu wa Serikali katika usimamizi wa rasilimali za Taifa.
Endapo Semu atapitisha na ACT-Wazalendo, atakuwa mwanamke wa pili ndani ya chama kuwania nafasi hiyo, wa kwanza alikuwa Hayati Anna Mghwira aliyepeperusha bendera ya chama hicho mwaka 2015, uliompa ushindi Hayati John Magufuli.
Siriwa na vipaumbele vitano
Februari 20, 2025, Siriwa alitangaza nia yake huku akibainisha vipaumbele vitano atakavyovitekeleza endapo atapeperusha bendera ya NLD na kushinda.
Kwa mujibu wa Siriwa, vipaumbele hivyo ni pamoja na elimu bure, afya bure, Katiba mpya, ajira kwa vijana na Tanzania ya kidijitali
Wakati makada hao wakijifua kwa mchuano, Katibu Mkuu wa UDP, Swaum Rashid amesema mchakato wa ndani chama hicho watautangaza hivi karibuni na kuwa tayari makada wameshaonyesha nia.
“Tunawasikia huko nje, lakini kwa taratibu za ndani ya chama bado. Watinia wapo lakini taratibu za chama rasmi kuhusu mchakato huu hazijaanza, ila zitaanza hivi karibuni,”amesema Rashid.
Maelezo ya Swaumu yalishaibiana na ya Husna Mohamed Abdallah, katibu mkuu wa CUF, aliyesema mchakato huo utaanza muda mfupi baada ya mwezi wa Mtukufu wa Ramadhan.
“Wapo walioonyesha nia kwa nafasi mbali mbali ikiwemo urais wa Zanzibar, baadhi ya maeneo uwakilishi, ubunge na udiwani,” amesema Husna.
Katibu Mkuu wa AAFP, Rashid Rai amesema kwa upande wa Zanzibar, Said Soud ametangaza nia ya kuwania urais, lakini kwa muungano bado hajajitokeza mtu ingawa milango ipo wazi.
Mwenyekiti wa Ada Tadea, Juma Ali Khatib, amesema wameshafungua pazia la kuchukua na kurejesha fomu sambamba na kuwaruhusu makada wa chama hicho, kutangaza nia.
“Tumeshafungua pazia la watu kutangaza nia na kuchukua fomu, mimi nimeshatangaza nia ya kuwania urais wa Zanzibar. Lakini tumeweka utaratibu utoaji wa fomu bure kwa wanawake na wenye mahitaji maalumu wanaotaka kuwania urais, ubunge na udiwani,” amesema Khatib.
Baadhi ya wasomi waliozungumza na Mwananchi wamesema vyama vilivyoanza mchakato huo mapema, vipo sahihi na vinakwenda na muda katika kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mohamed Bakari amesema pamoja na kwamba INEC haijatangaza rasmi utaratibu utakavyokuwa, lakini ili kuendana na muda vyama hivyo vipo sahihi.
“Kitu muhimu ni taarifa kuwafikia wapigakura ili wajue wagombea wao, unapokuwa na muda mfupi hauwezi kutoa fursa ya kutosha kwa wapiga kura kuwajua watia nia wao. Kutangaza nia mapema inasaidia sana kwa wapigakura na wale wanaotarajia kuteuliwa.
“Kuingia katika uchaguzi si suala rahisi, huwezi kukurupa mwezi mmoja au miwili ukaingia kwenye kinyang’anyiro, unahitaji maadalizi ya muda mrefu, hasa kwa wale wagombea wapya. Wale wanaoendelea huwa kila wakati wanajijenga kwa nafasi zao ili kuchaguliwa tena,” amesema Profesa Bakari.
Kuhusu Chadema kuwa kimya, Profesa Bakari amesema chama hicho, kina ajenda yake No Reforms No Election, akisema ni sehemu ya siasa, hivyo wanapochangamkia na kujipanga kusaka wagombea wataonekana wanakubaliana na mfumo wa uchaguzi uliopo.
“Kisiasa na kimkakati wao Chadema wameona wachelewe kidogo, huenda ikawasaidia kuendelea kusisitiza madai yao. Sasa wakionekana wanaanza kuteuana, wakati walishasema watazuia uchaguzi, wao kuchelewa wanaona sawa.
“Hata kama madai yao hayatakubaliwa lakini huenda yakatoa taswira miongoni mwa wanachama wao, kwamba walipambana na kushindwa,” amesema Profesa Bakari.
Mchambuzi wa mwingine wa siasa, Kiama Mwaimu amesema hatua za vyama za siasa kuanza mchakato huo mapema zinatoa wigo kwa watu kuwapima mapema walioanza kutia nia na kuchukua fomu.
“Wapo sahihi na muda ni mzuri wa kuangalia watu kwa miezi sita mingine ijayo, kabla ya kufanya uchaguzi. Wasiwasi wangu kwenye hivi vyama vya siasa, vitaweza kuwa kitu kimoja kwa njia isiyoleta mpasuko baada ya mchakato wa uteuzi kuisha?
“Mfano kilichotokea ndani ya Chadema, tumeona demokrasia imechukua nafasi yake, lakini inaonekana hali bado siyo nzuri, hasa ukisikia kauli za viongozi wao waliopo madarakani,”amedai Mwaimu.
Mwaimu amesema masuala hayo, yanaweza kusababisha kupunguza hata nguvu za mchakato wa mbio za kuwania urais kwa chama husika.
“Kwa ujumla wamejua kucheza vizuri na muda, hasa kwa watu tunaotafakari nani anaweza kufaa ambapo itatusaidia kuwaona mapema.Hofu yangu vyama vyenyewe ndivyo vitakavyosababisha matatizo katika uteuzi,”amesema Mwaimu.