Kanda ya Ziwa ilivyopindua meza mapato ya halmashauri

Kabla ya mwaka 2022 Kanda ya Dar es Salaam ilikuwa ukiongoza katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri nchini, ikiziacha mbali kanda nyingine tano.

Hata hivyo, mwaka 2023 ulikuja kivingine baada ya Kanda ya Ziwa kujinasua kutoka nyuma na kusimama kileleni katika orodha ya kanda zenye makusanyo makubwa ya mapato ya halmashauri.

Kanda ya Ziwa inajumuisha mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera, Simiyu, Geita na Shinyanga ambayo kwa pamoja ina jumla ya wakazi milioni 16.42, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, lakini kabla ya mwaka 2022 ilikuwa ikizidiwa na Dar es Salaam kwenye ukubwa wa mapato yanayokusanywa.

Kanda ya Dar es Salaam inajulikana kama eneo muhimu la kiuchumi kutokana na wingi wa biashara zinazofanyika na kwa muda mrefu imekuwa ikikusanya mapato mengi zaidi.

Ripoti ya Uchumi wa Kanda iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza kuwa katika robo ya mwaka ulioishia Septemba 2024, Kanda ya Ziwa ilifikisha mapato ya Sh74.8 bilioni, yakiongezeka kutoka Sh45.3 bilioni kipindi kama hicho mwaka 2021.

Ukusanyaji wa mapato uliofanyika mwaka jana unaifanya kanda hiyo kubeba asilimia 25.4 ya makusanyo ya kanda zote nchini kwa kipindi husika.

Kanda ya pili ni ya Kati, ambayo ilikuwa na makusanyo ya Sh56.6 bilioni, ikiwa ni ongezeko kutoka Sh32.6 bilioni Septemba 2021. Kanda hii ilishika nafasi hiyo kwa kukusanya mapato mengi ya halmashauri Septemba mwaka jana, ikibeba asilimia 19.2.

Dar es Salaam iliyozoea kuongoza, sasa inashika nafasi ya tatu ikikusanya Sh52.8 bilioni, ikiwa ni pungufu kutoka Sh54.2 bilioni Septemba 2021.

Jiji la Dar es Salaam ndilo namba moja kwa ukubwa wa pato la Taifa na makusanyo yake ya mwaka 2021 yaliifanya kanda yake kuwa kinara kabla ya kuanza kushushwa na Kanda ya Ziwa.

Licha ya uchache wa watu ambao Kanda ya Dar es Salaam ilikuwa nao katika mwaka 2021, iliweza kuzipiku kanda ambazo zina muunganiko wa mikoa kabla ya mikoa hiyo kuamka.

Hata hivyo, pamoja na uchache wa watu ukilinganisha na baadhi ya kanda, Dar es Salaam iko juu ya kanda za Kaskazini, Kusini Mashariki na Nyanda za Juu Kusini inayoshika mkia.

Kaskazini nayo imefanikiwa kuongeza ukusanyaji mapato kutoka Sh35.4 bilioni robo ya Septemba 2021 hadi Sh42.3 Septemba mwaka jana. Kusini Mashariki makusanyo yaliongezeka kutoka Sh23.9 bilioni hadi Sh45.6 bilioni katika kipindi hicho.

Hiyo ni tofauti kwa kanda ya Nyanda za Juu Kusini ambayo mapato yake walishuka kutoka Sh25.4 bilioni hadi Sh22.2 bilioni.

Kuimarika kwa makusanyo Kanda ya Ziwa kumechangiwa na usimamizi bora na kukua kwa shughuli za kiuchumi, kwa mujibu wa wachambuzi wa uchumi.

Mtaalamu wa Uchumi, Dk Donath Olomi amesema ukuaji huo ni jambo linalohitaji kuangaliwa vizuri, lakini huenda shughuli za madini zimeongezeka Kanda ya Ziwa na kuwa kichocheo cha ukuaji wa mapato ya halmashauri.

“Pia huenda ufuatiliaji umeongezeka, udhibiti wa wizi umeongezeka kwa sababu mapato hayo yamekuwa yakivuja kutokana na tabia za baadhi ya watumishi,” anasema Dk Olomi.

Dk Olomi ameongeza kuwa kuna uwezekano wa ongezeko la uuzaji wa mazao ya chakula na mifugo, ikizingatiwa kuwa Kanda ya Ziwa ina uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo.

Naye Mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude anasema ukuaji huu unaweza kuwa umechangiwa na uwekezaji wa miundombinu uliofanywa katika kanda hiyo unaovuta shughuli mbalimbali za kiuchumi. “Pia kuimarika kwa usimamizi katika makusanyo wenyewe, kunaweza kuwa na ukuaji lakini kama usimamizi haufanyiki ni kazi bure, maana kunakuwa na pengo linalopitisha vitu vingi,” anasema Mkude.

Anasema kwa Dar es Salaam kinachoonekana pengine kimechangiwa na matukio yaliyotokea ndani ya kipindi hicho, yaliyofanya baadhi ya shughuli kutofanya vyema kama ilivyokuwa awali.

Mbali na maoni hayo, Mchambuzi wa masuala ya uchumi na Biashara, Dk Balozi Morwa yeye anasema si Kanda ya Ziwa pekee, bali kanda nyingi zitazidi kuipiku Dar es Salaam.

Anasema matarajio yake ilikuwa ni kuona Kanda ya Kati inaipiku Dar es Salaam katika ukusanyaji wa mapato, kwa sababu Dodoma sasa ina mzunguko mkubwa wa fedha.

Dk Morwa anaamini kuwa Mkoa wa Dodoma sasa una shughuli nyingi za kiserikali ambazo zimesisimua shughuli mbalimbali za biashara, tofauti na zamani.

“Takwimu zina walakini, siamini kuwa Kanda ya Ziwa ndiyo imeipiku Dar es Salaam na Kanda ya Kati, si kweli … nashindwa kuamini kuwa kanda hii imepiku kanda nyingine zote, nashindwa kuamini…” anasema Dk Morwa.

Anasema shughuli za kiuchumi zilizopo katika kanda hiyo ni ndogo kuliko zinazoendelea maeneo mengine kama Dar es Salaam, Arusha na Dodoma.

“Tukisema wana madini, hayajaanza leo, yalikuwapo siku nyingi kwa nini haikuonekana, huenda kuna shida katika matumizi ya takwimu, lakini uhalisia ulivyo katika maeneo husika hauendani na takwimu husika kwa sababu shughuli za kiuchumi nyingi ziko Arusha, Mbeya, Dar es Salaam,” anasema.

Anasema ni vyema suala hilo kunafanyiwa utafiti wa kina ili kujua ni kitu gani kimechochea ongezeko hilo.

Related Posts