UONGOZI wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) umeipa ruhusa Yanga kwenda Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kupinga uamuzi wa kuahirishwa kwa mchezo wao dhidi ya Simba uliokuwa uchezwe Machi 08.
Yanga inaona uamuzi huo haujaitendea haki ikidai hakufuata kanuni na ulilenga kuibeba Simba iliyotangaza kutokuwa tayari kucheza kwa vile ilizuiwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, siku moja kabla.
Mwenyekiti wa TPLB, Steven Mnguto, ameliambia Mwanaspoti hawaizuii Yanga kwenda CAS, lakini walipaswa kusubiri hadi Bodi itoe uamuzi wa mwisho juu ya suala hilo.
“CAS huwezi kuzungumza tu, CAS ni rahisi lakini ina taratibu zake. Kwa sababu wenzetu walishawahi kwenda CAS kwa suala la Morrison (Bernard) sina shaka wanajua hizo taratibu na watazipitia hizo taratibu kwa hiyo kama wanaenda CAS, leo huwezi kumkataza mtu, kubwa sisi ni kuja kujibu kama tutaitwa na CAS kwenda kujibu na tunayo majibu na wakati huo kama tumeshafanya maamuzi yetu tutapeleka kwamba maamuzi yetu ni hivi,” alisema Mnguto.
Hata hivyo, Yanga inaripotiwa tayari imeshapeleka malalamiko yao, CAS yakiambatana na kiasi cha Dola 40,000 (Sh106 milioni) ambayo ni ada ya kuendeshea kesi hiyo.
Wakati Yanga ikisubiri kufahamu tarehe ya kusikilizwa kwa shauri hilo pamoja na jopo la wasuluhishi, muongozo wa uendeshaji mashauri wa CAS unampa mamlaka Mfaransa, Carole Malinvaud wa kuamua ni lini na kina nani watamaliza mjadala juu ya suala hilo.
Idadi ya wasuluhishi inaweza kuanzia mmoja hadi watatu na wanachaguliwa na Rais wa Kitengo husika ambaye kwa sasa ni Malinvaud.
“Rais wa Kitengo ataamua nambari hiyo, kwa kuzingatia mazingira ya kesi hiyo. Kisha Rais wa kitengo anaweza kuchagua kuteua msuluhishi pekee wakati mlalamishi anapoomba hivyo na mlalamikiwa hatalipa sehemu yake ya malipo ya awali ya gharama ndani ya muda uliowekwa na Ofisi ya Mahakama ya CAS,” imefafanua ibara ya 40.1 ya muongozo wa CAS.
Malinvaud ni gwiji wa Sheria za kimataifa za biashara na pia usuluhishi wa migogoro. Ni mhitimu wa vyuo maarufu vya sheria vya Paris II Ufaransa na Shule ya Sheria ya Havard, Marekani.
Kwa sasa ni Mwenyekiti wa Tume ya Kimataifa ya usuluhishi wa kibiashara ya Ufaransa aliyohudumu kuanzia 2013 na pia amewahi kuwa mwenyekiti wa kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Mchezo wa Gofu.
Malinvaud atateua msuluhishi/wasuluhishi kutoka kundi la wasuluhishi 171 wa Cas ambao miongoni mwao kuna Waafrika saba.
Waafrika wanaoweza kuteuliwa kuamua suala la Yanga ni Tshiamo Rantao na Terence Dambe (Botswana), Paul Pretorius, Tembeka Ngcukaitobi na Poobalan Govindasamy (Afrika Kusini), Wellington Magaya (Zimbabwe) pamoja na Abdallah Shehata wa Misri.
KESI KAMA HIYO ILIAMULIWA 2018
Kitendo cha Yanga kwenda CAS kudai haki yao, inaturudisha nyuma hadi mwaka 2018 walipofanya hivyo Boca Juniors ya Argentina waliokuwa na mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Amerika ya Kusini dhidi ya River Plate pia ya Argentina.
Timu hizi zenye upinzani wa muda muda mrefu kama ilivyokuwa Yanga na Simba, lakini wao mara nyingi mechi zao zimekuwa zikigubikwa na matukio mengi ya vurugu kutokana na ushindani huo.
Mchezo wa mkondo wa kwanza wa fainali hiyo ulipigwa Novemba 11, 2018, ukamalizika kwa sare ya 2-2, kisha marudiano ukapangwa kupigwa Novemba 24, 2018.
Hata hivyo, mchezo huo haukufanyika kwa sababu ya vurugu zilizozuka nje ya uwanja zilizosababisha basi la wachezaji wa Boca Juniors kushambuliwa na baadhi yao kuumizwa na mwishowe wakaondoka katika eneo la uwanja wa mchezo huo.
Kutokana na hali hiyo, Shirikisho la Soka Amerika ya Kusini (CONNMEBOL), likaahirisha mchezo huo na kupanga tarehe nyingine, huku ikiamuliwa mechi hiyo itapigwa nje ya Argentina.
Boca Juniors walipinga suala hilo na kusisitiza hawatocheza mechi hiyo, wakaenda mbali zaidi wakifunguka kwamba River Plate haikutakiwa kushiriki kabisa mechi hiyo kutokana na vitendo vyao, hivyo wao wapewe ushindi wa mezani na ikiwa hawatosikilizwa watapeleka kesi hiyo kwenda Mahakama ya Usuluhishi wa Masuala ya Michezo (CAS).
Hata hivyo, CONNMEBOL ilitupilia mbali shauri hilo na baada ya hapo, Boca iliwasilisha kesi kwenda CAS ambako pia waligonga mwamba.
Mwisho mechi hiyo ikaenda kupigwa Desemba 9, 2018 kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu, Hispania ambapo River Plate ilishinda kwa mabao 3-1, hivyo ikaibuka bingwa kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-2 na kubeba ndoo ya michuano hiyo.