MSD yasema SPPS ipo palepale

Dodoma. Nchi za Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (SADC) zimefumua upya mpango wa ununuzi wa pamoja wa bidhaa za afya (SPPS), unaoratibiwa na Tanzania chini ya Bohari ya Dawa (MSD), ili kuondoa changamoto zilizokuwepo awali.

Makubaliano hayo yalifikiwa Novemba Mwaka 2017, mawaziri wa afya wa SADC na mawaziri wanaohusika na VVU na Ukimwi wakati wa mkutano wao wa kikanda uliofanyika Polokwane nchini Afrika Kusini.

Katika mkutano huo, waliidhinisha Tanzania kupitia Bohari ya Dawa (MSD) kushughulikia huduma za SPPS kwa nchi 16 za wanachama wa SADC ambazo zina wastani wa watu milioni 346.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai ameyasema hayo jana Jumatano Machi 19, 2025 wakati akizungumzia mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita na mwelekeo wa bohari hiyo.

“Baadaye tukaanza ‘revival’ (kuutengeneza upya) ya mpango, sasa ni kama kufufua kitu ambacho kilishatuama. Na mnakumbuka tulipotoka katika Uviko-19 kila mtu alianza kujipambania mwenyewe apone, sisi tukaingia katika viwanda vyetu na ununuzi upya,” amesema.

Amesema mwaka 2023/24 walifanya utafiti wa kuona wanauanza vipi upya kwa sababu ulikuwa na changamoto tano ambazo ni nchi kuwa fursa ya kufanya uchaguzi wa kununua ama kutonunua, sheria za ununuzi, sheria za fedha ambapo kila nchi ilikuwa na utaratibu wake wa kununua bidhaa.

Nyingine ni utaratibu mamlaka za udhibiti wa ubora wa bidhaa za afya za nchi zilizopo katika jumuiya hiyo na bidhaa ambazo zilikuwa zimewekwa katika  mpango wa kwanza ya ununuzi ambazo nyingi zilikuwa ni za kawaida.

Amesema changamoto nyingine hakukuwa na mfumo wa manunuzi wa pamoja na kwamba sasa hivi wanatengeneza Mfumo wa Kieletroniki wa Ugavi wa SADC (ESPPS).

“Sasa hivi tunaweka mfumo uendane na matakwa ya kimataifa, kwa hiyo tumetengeneza ‘business plan’ mpya ilipitishwa na kikao maalumu cha wajumbe wa SADC na yameshatolewa maelekezo ya utekelezaji,” amesema.

Tukai amesema kuwa watakwenda kufanya ununuzi wa pamoja kwa bidhaa ambazo wanapata nazo shida katika manunuzi kutokana na matumizi yake kuwa madogo.

Pia, MSD imesema kwa kutumia kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na balozi mbalimbali inaendelea na jitihada za kuvutia uwekezaji kwenye bidhaa za afya ikiwemo dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi (ARV) na mipira ya kiume.

Tukai amesema kupitia kampuni tanzu, MSD itaendelea na jitihada za kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza idadi ya viwanda vya bidhaa za afya nchini hivyo kupunguza matumizi ya fedha za kigeni.

Amesema MSD inaendelea kutumia TIC na balozi zetu ili kuweza kuvutia wawekezaji wenye lengo la kufanya uzalishaji nchini.

“Jitihada hizi zinafanyika kwenye uwekezaji kwenye bidhaa za ARV, mipira ya kiume (Condoms), bidhaa za afya zitokanazo na pamba, dawa mchanganyiko na bidhaa nyinginezo,” amesema.

Aidha, Tukai amesema Serikali kupitia MSD inatekeleza mpango maalumu wa kuongeza upatikanaji wa huduma za uchujaji wa damu ikiwa ni sehemu ya matibabu ya figo, hivyo kupunguza gharama za huduma hiyo.

Amesema kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya awamu ya sita, hadi kufikia Februari 2025, idadi ya mashine imeongezeka na kufikia 137 kutoka 60.

Amesema hilo limeongeza idadi ya hospitali zilizopokea mashine kutoka Bohari ya Dawa kutoka sita zilizokuwepo mwaka wa fedha 2021/22 na kufikia 15 mwaka 2024/25.

Kuhusu usambazaji wa mashine za dialysis amesema unalenga kupunguza gharama ambapo kwa sasa zinazotozwa ni kati ya Sh200,000 na Sh230,000 na matarajio ni kupunguza na kuwa chini ya Sh100,000 kwa ‘session’ moja.

Mkazi wa Dodoma Mjini, Sostenes Edwin ameiomba Serikali kuongeza upatikanaji wa dawa katika hospitali za umma ili kuondoa usumbufu kwa wagonjwa.

“Ukienda hospitali bado kuna shida ya upatikanaji wa dawa, unaweza kuambiwa hii haipo nenda kanunue ulete, ukiangalia wakati mwingine huna fedha mfukoni,”amesema.

Related Posts