Mwanza. Mwanamke mmoja ambaye bado hajafahamika, amekutwa amefariki dunia katika chumba cha nyumba ya wageni eneo la Usagara, Wilaya ya Misungwi jijini hapa.
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa iliyotolewa jioni ya jana Jumatano Machi 19, 2025 imeeleza kuwa mwanamke huyo alikutwa amefariki dunia kwenye chumba namba tatu katika nyumba hiyo inayojulika kwa jina la First and Last guest.
Mutafungwa amesema baada jeshi hilo kufika katika eneo la tukio jana, walibaini Machi 18, 2025 saa 1 jioni alifika mgeni katika nyumba hiyo aliyejiandikisha kwa jina la Bilal William, mkazi wa Geita akitokea Chato kuelekea Nzega mkoani Tabora.
Amesema mgeni huyo alipewa chumba namba tatu na kuweka mizigo yake, ilipofika saa nne usiku alitoka chumbani akidai anakwenda kutafuta chakula na ilipofika usiku mkubwa mwanaume huyo alirudi katika nyumba hiyo ya kulala wageni akiwa na mwanamke.
“Inadaiwa ilipofika saa 12:00 asubuhi wakati wahudumu wa nyumba hiyo ya kulala wageni wakihitaji kufanya usafi ndipo walipokuta mlango wa chumba hicho ukiwa na komeo lililofungwa kwa nje hali hiyo iliwatia mashaka, hivyo kufungua kufuli hilo na kuingia ndani, na ndipo walipoona kuna mwanamke amefungwa usoni kwa kitambaa pamoja na mikwaruzo usoni mwake huku akiwa mtupu ambapo mwanaume aliyepangisha chumba hicho hakuwepo,” amesema Mutafungwa
Amesema mwili wa marehemu umepelekwa Hospitali ya Wilaya ya Misungwi kwa ajili wa uchunguzi licha ya kuwa bado haujatambulika hadi sasa.
“Hivyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawataka watu wa maeneo ya karibu na tukio hilo lilipotokea kufika hospitali ya Misungwi kuuona mwili huo kwa ajili ya utambuzi. Uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini chanzo chake pamoja na kumkamata mtuhumiwa huyo,” amesema.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Miembeni, Nubi Ubwakala amesema alipewa taarifa na wahudumu wawili wa nyumba hiyo kwa njia ya simu wakimueleza marehemu akiwa na mwanaume huyo walikwenda kwenye nyumba hiyo kwa ajili ya kupumzika.
Amesema baada ya kupata taarifa hiyo alifika eneo la tukio kisha kusimuliwa jinsi ilivyokuwa na kumtaarifu Mtendaji wa Kata na Jeshi la Polisi waliofika kwa wakati na kuanza kufanya majukumu yao.
“Kulikuwa na watu wengi wamekusanyika…wakautoa mwili nje ili kuwaruhusu watu waliokuwapo nje waangalie ule mwili pengine wanaweza wakautambua lakini hakuna aliyemtambua hata mmoja. “Hata sisi viongozi maana tulikuwa na kamati ya ulinzi na usalama ya kijiji hiki pia na wao hawakutambua hiyo sura ya marehemu,” amesema.
Mwakilishi wa mmiliki wa nyumba hiyo ya kulala wageni, Jemy Kilala amesema hajui nini kilitokea hadi marehemu hakuandikishwa jina kwenye kitabu cha wageni, kwani kiutaratibu hata yeye alipaswa kupita mapokezi kwa ajili ya taarifa zake kurekodiwa.
Naye, shuhuda wa tukio hilo ambaye ni mfanyabiashara wa duka jirani na nyumba hiyo ya wageni, Ayubu Kipenya amesema: “Ni tukio lililotusikitisha, maana ni mama mtu mzima aliyefanyiwa unyama sasa sijui huyo aliyefanya hicho kitendo alikuwa na nia gani…ni kitu ambacho kinaumiza na kinaleta hisia mbaya kwa sisi tunaokaa maeneo haya.”
Amesema licha ya wananchi kupewa nafasi ya kumtambua mama huyo aliyedai alikuwa ‘mtu mzima’ lakini hawakufahamu mahali anapoishi japo walishawahi kumuona maeneo hayo.