Rais Samia mgeni rasmi kuapishwa Rais wa Namibia

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi katika Jamhuri ya Namibia kesho Ijumaa Machi 21, 2025 kuhudhuria sherehe za uapisho wa Rais mteule wa nchi hiyo, Netumbo Nandi-Ndaitwah.

Rais Samia amealikwa kama mgeni rasmi na anatarajia kuhutubia kwenye sherehe hizo za uapisho zitakazofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 35 ya uhuru wa Namibia.

Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Sharifa Nyanga leo Alhamisi Machi 20, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mahusiano baina ya Tanzania na Namibia yaliasisiwa na hayati Julius Nyerere na hayati Sam Nujoma kipindi cha harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa bara la Afrika.

“Mahusiano haya yameendelea kukuzwa na kulelewa na viongozi wote wakuu waliowafuatia katika nyanja mbalimbali,” imeeleza taarifa hiyo.

Mbali na kuhudhuria sherehe hizo, Rais Samia atapata fursa ya kusalimiana na mwenyeji wake na kufanya mazungumzo ya kukuza na kuimarisha mahusiano.

Kwa mara ya kwanza Namibia itapata rais mwanamke hivyo kufanya idadi ya marais wanawake barani Afrika kuwa wawili akiwemo Rais Samia.

Ndemupelila anakuwa rais wa awamu ya tano wa Namibia na wa kwanza mwanamke katika nchi hiyo, baada ya kushinda kwenye uchaguzi mkuu kwa kupata asilimia 57, akimshinda mpinzani wake, Panduleni Itula wa IPC aliyepata asilimia 26 ya kura zote.

Mshindi huyo ameendeleza utawala wa chama cha Swapo kilichopigania uhuru wa nchi hiyo na kuwezesha kupata uhuru mwaka 1990 kutoka kwa utawala uliokuwa wa makaburu wa Afrika Kusini.

Kabla ya kugombea nafasi hiyo, Nandi-Ndaitwah alikuwa makamu wa tatu wa rais wa Namibia tangu Februari 2024. Mwaka 2017, alichaguliwa kuwa makamu wa rais wa Swapo, mwanamke wa kwanza kushika nafasi hiyo.

Netumbo Nandi alizaliwa Oktoba 29, 1952 Onamutai, Ovamboland, Afrika ya Kusini Magharibi (ambayo leo ni Mkoa wa Ohangwena, kaskazini mwa Namibia). Baba yake alikuwa kasisi wa Kanisa la Anglikana.

Ni mtoto wa tisa kati ya watoto 13 wa familia yao.

Related Posts