Russia, Ukraine zabadilishana wafungwa 372 wa kivita

Kyiv.  Ukraine na Russia zimefanya mabadilishano ya wafungwa wa kivita 372 kupitia mpango ulioratibiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Wizara ya Ulinzi ya Russia imethibitisha kuwaachilia wanajeshi 175 na wafungwa 22 wa Ukraine waliojeruhiwa vibaya na wanaohitaji msaada wa haraka wa matibabu kwenda kuungana na wapendwa wao nchini Ukraine.

Shirika la Habari la Associated Press limeripoti kuwa kupitia mabadilishano hayo yaliyofanyika jana Jumatano, Russia ilisema kuwa Ukraine iliwaachilia huru wanajeshi 175 wa Russia waliokuwa wamewekwa kizuizini kama wafungwa wa kivita chini ya utawala wa Rais Volodymyr Zelensky.

Rais Zelenskyy naye amethibitisha ubadilishanaji huo. Kupitia chapisho lake kwenye mtandao wa X, Zelensky ameandika; “Ilikuwa moja ya mabadilishano makubwa zaidi tangu Russia ilipoanzisha uvamizi wake wa kijeshi nchini Ukraine Februari 2022,”

Mabadilishano hayo yamefanyika baada ya Jeshi la Ukraine kudai kuwa Russia ilirusha ndege zisizo na rubani (droni) 145, ambapo mifumo ya ulinzi wa anga ya Ukraine ilidungua 72 kati ya hizo.

Wizara ya Ulinzi ya Ukraine pia ilisema mtu mmoja aliuawa na hospitali mbili ziliharibiwa kutokana na mashambulizi hayo ya Russia, ambayo pia yaliathiri usambazaji wa umeme kwenye baadhi ya njia za reli nchini humo.

Kwa upande wake, Wizara ya Ulinzi ya Russia ilisema kuwa mifumo yake ya ulinzi wa anga iliangusha droni 57 za Ukraine.

Katika eneo la kusini mwa Russia la Krasnodar, mamlaka zilisema kuwa shambulio la droni la Ukraine lilisababisha moto katika kituo cha mafuta karibu na kijiji cha Kavkazskaya, ingawa hakuna mtu aliyejeruhiwa.

Wakati hayo yakijiri, Rais wa Marekani, Donald Trump amemwambia Rais Zelenskyy kuwa Marekani inapaswa kuchukua umiliki wa mitambo ya nishati ya Ukraine ili kuimarishia ulinzi dhidi ya mashambulizi ya Russia.

Hata hivyo, Rais Zelenskyy ameonyesha kuunga mkono pendekezo hilo na kusema Ukraine iko tayari kwa sharti ya kuimarishiwa ulinzi wa miundombinu yake ya nishati.

Haijabainika mara moja ni mitambo ipi ya nishati inayotakiwa kuwekwa chini ya udhibiti wa Marekani katika mazungumzo hayo.

Kauli hiyo ilitoka baada ya mazungumzo ya simu yenye matokeo chanya kati ya Zelensky na Trump, siku moja baada ya kuzungumza kwenye simu kwa saa mbili na Rais wa Russia, Vladimir Putin.

Zelensky na Trump walizungumza jana Jumatano kwa takriban saa moja, huku Trump akiendelea na juhudi zake za kuhakikisha usitishaji mapigano kati ya pande hizo unafanikiwa.

Baada ya simu hiyo, Trump aliandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa alifanya mazungumzo mazuri sana na Zelenskyy na juhudi za kufanikisha makubaliano ya kusitisha mapigano zinaendelea vizuri.

Wakati wa mazungumzo yake na Putin siku ya Jumanne, kiongozi wa Russia alikubali kutochukua tena hatua za kijeshi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Ukraine, lakini alikataa kuunga mkono usitishaji mapigano wa siku 30 kwa ukamilifu.

Katika ujumbe wa mtandaoni, Zelenskyy alisema kuwa mazungumzo yake na Trump yalikuwa chanya ya kina na ya wazi, huku akiongeza kuwa anaamini amani ya kudumu inaweza kupatikana mwaka huu kwa msaada wa Marekani.

Zelenskyy alisema kuwa Ukraine itaendelea kufanya kazi ili kufanikisha usitishaji wa mapigano huku akiweka wazi, “kutakuwa na mikutano zaidi siku zijazo nchini Saudi Arabia kati ya timu za Marekani na Ukraine.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Related Posts