Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitarajia kufanya sensa ya uzalishaji viwandani mwaka huu, wamiliki wametakiwa kutoa ushirikiano unaohitajika kufanikisha kazi hiyo.
Mara ya mwisho sensa ya aina hiyo ilifanyika mwaka 2013 iliyoonyesha idadi ya viwanda vilivyokuwepo ni 49,243 ndani yake vikiwamo vidogo kabisa, vidogo, vya kati na vikubwa.
Sensa hiyo itakusanya taarifa muhimu za kiwanda, bidhaa zinazozalishwa na aina ya umiliki, ajira, gharama za ajira na uzalishaji, bidhaa zilizozalishwa na mauzo, thamani ya mali zilizopo ghalani mwanzoni na mwishoni wa mwaka, thamani ya rasilimali zisizohamishika na taarifa nyingine mtambuka.
Akizungumzia sababu za kufanyika sensa hiyo leo Machi 20, 2025 katika mkutano na wenye viwanda mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Amina Msengwa amesema mahitaji ya takwimu sahihi, zinazokwenda na wakati na za kuaminika ni muhimu ili kuhakikisha nchi inapiga hatua kubwa na kufikia uchumi wa kati ngazi ya juu kuhakikisha maendeleo endelevu.
“Katika dunia ya leo yenye fursa nyingi na inayobadilika kwa kasi, Serikali haiwezi kuhuisha sera, kupanga na kutoa uamuzi bila kuwa na takwimu sahihi za wakati uliopo,” amesema.
Dk Amina amesema viwanda vinapoongezeka na kupanuka, mazingira yanayozunguka Taifa yanapoendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali za kiushindani ni muhimu kuandaa mikakati ya ndani ya nchi kwa kutumia takwimu sahihi na zinazoenda na wakati.
Amesema takwimu ni nyenzo ya kufanya uamuzi wenye ufanisi, unaotoa fursa ya kutathmini athari, kutambua fursa, kuboresha na kupima utendaji katika sekta mbalimbali.
Amesema zinasaidia kutoa mwelekeo wa masoko na kutabiri mahitaji ya watumiaji, hivyo takwimu ni msingi wa kufanya tathmini yenye tija katika ukuaji wa sekta za uchumi.
Amesema kuna mabadiliko mengi yametokea katika sekta ya viwanda kwa kipindi cha miaka 10, hivyo ni vema fursa hiyo ikatumika kufanya sensa ya uzalishaji viwandani ya mwaka 2025 kwa rejea ya 2023, lengo likiwa kutathmini maendeleo yaliyopatikana katika kipindi hicho.
“Nawahakikishia wamiliki wa viwanda kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu, taarifa zote zinazokusanywa katika sensa na tafiti za kitakwimu ni siri na zinatumika kwa madhumuni ya kitakwimu pekee. Katika kuhakikisha usiri wa taarifa, wadadisi baada ya kufaulu mafunzo ya mbinu za utafiti wamekula kiapo cha kutunza taarifa hizo na makosa ya kutotunza siri yana adhabu ya kifungo na faini,” amesema.
Dk Amina amesema suala la uzalishaji wa takwimu ni jumuishi, si la Ofisi ya Taifa ya Takwimu pekee, hivyo inahitaji ushirikiano na wadau mbalimbali katika ngazi zote za kiutawala na wananchi, ambao ndio watoa taarifa katika sensa na tafiti.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo amesema ushiriki wa wenye viwanda ni muhimu kwa ajili ya kuona nchi imefikia wapi ili kwenda na wakati.
Amebainisha changamoto zilizojitokeza kwenye sensa iliyopita ni maofisa waliokusanya taarifa kuzuiwa, kuchelewesha dodoso, kutoa taarifa za uongo na wengine kukataa kutoa taarifa.
Dk Jafo amesema Taifa lolote lazima liwe na takwimu za sehemu mbalimbali ili sera na mikakati inayoandaliwa iwe na sehemu ya marejeo ya mipango.
Amesema sensa itakayofanyika itasaidia kujua bidhaa zinazozalishwa kwa wingi na kuweka misingi mizuri ya kisera, kikanuni na sheria ili kulinda viwanda nchini.
“Tukifanya sensa hii tutaona hali ikoje kwenye viwanda vya ndani na kama vinazalisha vizuri hakutakuwa na haja ya kuagiza bidhaa kutoka nje,” amesema.
Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Anne Makinda amewataka wenye viwanda kutoa ushirikiano pindi maofisa watakapofika kwao, akisema wamepata mafunzo na wanafanya kazi kwa usiri.
“Ndugu zangu wenye viwanda naomba muwape ushirikiano wa kutosha wakusanya taarifa, umuhimu wa sensa hii itasaidia kupata taarifa zilizo sahihi kwa ajili ya kujua nchi inaenda wapi na kusaidia watunga sheria na sera kuweka vitu kwa misingi iliyo sahihi,” amesema.