Mbeya. Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amesema licha ya kutokuwa sehemu ya maamuzi ya kugawa jimbo hilo, lakini ni miongoni mwa wanaosubiri mchakato huo kukamilika, huku akikanusha taarifa za kuwa hatagombea.
Pia, amesisitiza kuwa anachosubiri ni uamuzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuligawa jimbo hilo linaloongozwa na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ili ajue atagombea wapi.
Mbeya ni miongoni mwa mikoa iliyopendekeza majimbo yake matatu kugawanywa ikiwa ni Mbeya Mjini ili kupata jimbo jipya la Uyole, Mbeya Vijijini Mbalizi na Mbarali.
Akizungumza leo Machi 20, 2025 Sugu amesema mchakato unaoendelea wa kugawa jimbo hilo, anasubiri matokeo yake kwa kuwa hashiriki vikao vya namna yoyote vya maamuzi.
Sugu amesema kwa sasa ameamua kuwa mtulivu akisubiri wagawe ili kuona mpira ukifika uwanjani kuamua ni mguu wa kushoto au kulia wa kupigia danadana, huku akikanusha vikali taarifa zilizomtaja kuwa hatagombea.
“Mimi siyo mbunge, siingii kwenye vikao hivyo vya maamuzi, nasubiri matokeo ili kujua ni mguu upi wa kushoto au kulia wa kupigia danadana, kwa sasa nimekuwa mtulivu nikisubiri matokeo.
“Ndio maana tunapushi ‘No Reforms No Election’, lengo ni kugombea vinginevyo tungeweza kufanya shughuli nyingine kama kuuza chai na maandazi huko Desideria, ile posti iliyosambaa mitandaoni siyo ya kwangu” amesema Sugu.
Hata hivyo, kwa kipindi cha nyuma wakati wa mikutano yake Sugu, mara kadhaa alikaririwa akieleza kuhitaji kumfuata mbunge wa CCM, Dk Tulia popote atakapogombea kwenye uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.