Dodoma. Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) iliyopo jijini hapa imefanya operesheni ya kwanza ya ubongo kwa kutumia teknolojia ya mawimbi ya sauti (High-intensity Focused Ultrasound -HIFU) na kufanikiwa kutoa damu iliyokuwa imevilia kwenye ubongo wa mgonjwa.
Akizungumza leo Alhamisi Machi 20, 2025, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu ambaye aliongoza jopo la madaktari waliofanya upasuaji huo, Dk Maxigama Ndosi amesema wamefanikiwa kutibu mvilio wa damu kwenye ubongo wa mgonjwa kwa kusaidiwa na teknolojia ya mawimbi ya sauti.
“Hospitali ya Benjamini Mkapa imeanza kwa mara ya kwanza, matumizi ya mawimbi ya sauti kwa upasuaji wa kutoa damu na uvimbe kwenye ubongo (High-intensity Focused Ultrasound -HIFU), teknolojia hii inasaidia kufungua sehemu ndogo ya kichwa na kumuacha mgonjwa na kovu dogo ambalo linapona kwa haraka,” amebainisha Dk Ndosi.
Amesema kuwa utaalamu wa kutumia mawimbi ya sauti utasaidia kupunguza muda wa upasuaji kwa wagonjwa ambao wana damu kichwani na wenye uvimbe ndani ya ubongo.
“Teknolojia hii inasaidia katika upasuaji wa ubongo uwe wa kuondoa damu iliyovia kwenye ubongo kichwani au uvimbe kwa ajili ya saratani au wa namna nyingine na pia inaongeza ufanisi katika kufanya upasuaji ndani ya kichwa” amesema Dk Ndosi.

“Maana yake tunaweza kusema mtu yeyote anayekuja hapa BMH mwenye changamoto kama hiyo na ujuzi huu tulionao (Teknolojia ya kutumia mawimbi ya sauti wakati wa upasuaji wa ubongo) utakaotumika kumtibu, miaka yote sisi BMH tutakuwa mbele katika kufanya operesheni hizi kwa ufanisi zaidi,” amesema.
Naye Dk Kelvin Noel kutoka Idara ya Upasuaji Ubongo na Mishipa ya Fahamu hospitalini hapo, amesema baada ya kumpokea mgonjwa, walimfanyia vipimo na kubaini kuwa mbali na kupata tatizo la kiharusi (Stroke) damu ilikuwa imevilia kwenye ubongo wake, hali ambayo ingehatarisha uhai wa mgonjwa endapo asingepata matibabu kwa haraka.
“Jopo la madaktari lilijadiliana na kuamua kumfanyia upasuaji wa teknolojia hiyo ya mawimbi ya sauti na kufanikiwa kutoa damu yenye ujazo wa mililita 120 iliyokuwa imevilia kwenye ubongo.”
Kwa upande wake Issa Kassimu ambaye ni ndugu wa mgonjwa aliyefanyiwa operesheni hiyo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma za kisasa za afya, vifaatiba na wataalamu wenye uwezo wa kutoa huduma za kibingwa.