Walio sekta isiyo rasmi waanza kusajiliwa

Dar es Salaam. Wakati kutanua wigo wa wawalipa kodi ikiwa moja ya jambo linalopigiwa chapuo, Serikali imeanza kuwasajili watu wanaofanya shughuli zao katika mfumo usiokuwa rasmi.

Hiyo inajumuisha wafanyabiashara, wazalishaji, wachuuzi na watoa huduma mbalimbali waliopo nchini kupitia tovuti maalumu ya Vibindo Tanzania.

Vibindo Tanzania ni jumuiya inayokusanya vikundi 748 kutoka maeneo mbalimbali nchini ambapo ndani yake wapo pia wakulima na wafugaji wa nyuki.

Kuzinduliwa kwa usajili huu unatajwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) kuwa utachochea ongezeko la thamani la biashara hizo, kwani sasa itawaongezea nafasi ya kupata mikopo katika maeneo mbalimbali kutokana na kutambuliwa. 

“Utafiti wa nguvu kazi wa mwaka wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu 2020/2021 ulibainisha umuhimu mkubwa wa sekta isiyo rasmi katika kukuza ajira ukiwa unachangia asilimia 29 ya ajira zote, kiwango hiki ni kikubwa kwani ni sawa na waajiriwa 30 katika kila waajiriwa 100,” amesema Glory Blasio Mwakilishi wa ILO ofisi ya Tanzania.

Mchango wake katika ajira pia unashuhudiwa katika mapato ambapo utafiti wa NBS wa mwaka 2019 unaonyesha kuwa sekta hiyo inachangia asilimia 22.5 ya pato la mkoa wa Dar es Salaam.

“Takwimu hizi zinaonyesha kwa namna gani urasimishaji ni suala la muhimu, hivyo ni vyema kusimamia mchakato mzima wa mabadiliko na kuhakikisha utendaji unakuwapo ili kuondoa urasimishaji wa kwenye makaratasi,” amesema.

Kwa waajiri urasimishaji huchochea ukuaji na uendelevu wa biashara huku kwa wafanyakazi faida yake ikiwa ni kuleta ajira zenye staha, usalama wa ajira, kipato cha uhakika ambavyo kwa pamoja huenda sambamba na kuzingatia masuala ya hifadhi ya jamii na bima za afya.

Akizungumza baada ya kuzindua tovuti hiyo, Ofisa biashara mkuu ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Thabiti Massa ametaka tovuti hiyo kuunganishwa na tovuti nyingine zinazoweza kuwafanya watumiaji kufikia fursa za masoko kwa urahisi wakiwa ndani yake.

“Fursa hizo zitafikiwa kwa kuangalia mtu anauza nini huku akitolea mfano wa uunganishaji wa tovuti ya wizara ya kilimo ili kusaidia watu wanaolima mazao ya vyakula kujua bei, masoko mapya yanapopatikana,” amesema.

Pia alitoa rai kuangaliwa namna ambayo inaweza kusaidia kupunguza gharama hizo za usajili zinazotozwa kwa vikundi kutoka Sh95,000 iliyopo sasa.

Mwenyekiti wa Vibindo, Gaston Kikuwi amesema kusajiliwa kwao kutakwenda kuwasaidia kupata mitaji, maeneo rasmi ya kufanyia biashara, kupata huduma za hifadhi ya jamii, mafunzo yanayoendana na shughuli zao na teknolojia inayochukua nafasi kubwa katika jamii.

Oktoba 4, 2024 wakati wa uzinduzi wa Tume ya Rais ya maboresho ya kodi, Rais Samia Suluhu Hassan alisema kila anayestahili kulipa kodi nchini anapaswa kufanya hivyo, kwani sasa walipa kodi ni wachache na makusanyo hayaendani na viashiria vingine vya ukuaji wa nchi.

“Ni watu kama milioni mbili kati ya 65 milioni wanaolipa kodi, ukitoa watoto na wengine ambao hawapaswi kukatwa kodi hatupungui milioni 37… ina maana watu kidogo wanalipa kuwajenga watu wengi, hatuwezi kufika. Lazima wote tuchangie kila mtu na kiasi chake,” alisema Rais Samia katika hafla hiyo.

Related Posts