Arusha. Mahakama ya Rufani imemuachia huru Masenga Mwita, aliyekuwa amehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya kumuua aliyekuwa mkewe, Joyce Julius.
Masenga alihukumiwa na Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Julai 15, 2022, kutokana na kesi ya mauaji iliyokuwa ikimkabili.
Katika kesi hiyo, Masenga alidaiwa kumuua mkewe Februari 9, 2019 katika Kijiji cha Bukabwa wilayani Butiama, Mkoa wa Mara ambapo alidaiwa kumuua kwa kumnyonga na kumkata na sime kichwani kisha kwenda kutelekeza mwili wake uliokukutwa kando ya Mto Mara akiwa na jeraha la kukatwa kichwani.
Hukumu hiyo ya rufaa iliyomuachia huru imetolewa Machi 19, 2025 na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani wakiongozwa na Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma, Dk Mary Levira na Benhajj Shaaban Masoud.
Majaji hao walifikia uamuzi huo baada ya kupitia mwenendo wa kesi na kusikiliza hoja za pande zote mbili na kubaini kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka haukuweza kuthibitisha pasipo kuacha shaka kuwa Masenga alitenda kosa hilo.
Katika Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Masenga alipandishwa kizimbani kwa mauaji ya mkewe.
Kesi hiyo ilitokana na ushahidi wa shahidi wa tano ambaye alikuwa mtoto wa mrufani mwenye umri wa miaka minne, Chacha Masenga alidai Februari 8, 2019 alikwenda na mama yake Butiama kumtembelea baba yake (mrufani) na kuwa walipofika walimkuta mrufani, mama yake wa kambo na mtu mwingine.
Alidai walilala katika nyumba ya pembeni ambapo baba yake na mama yake wa kambo walilala nyumba nyingine iliyokuwa na umbali wa mita kama nane kutoka walipokuwa wamelala na mama yake.
Mtoto huyo alidai kuwa chumba walichokuwa wamelala na mama yake mlango ulikuwa umefungwa kwa jiwe na kuwa alimuona baba yake akiingia katika chumba hicho akiwa na sime na tochi iliyokuwa na mwana mkali na kuanza kumshambulia mama yake kichwani.
Alidai baada ya kumshambulia, baba yake alimbeba mama yake begani hadi nje ambapo alimuona akichukua baiskeli na kutokomea kusikojulikana na baada ya muda alirejea na kumchukua (mtoto huyo) hadi chumba kingine kulala.
Alidai siku iliyofuata mrufani alimtuma kwa bibi yake (mama wa mrufani) na kuwa siku ambayo haikumbuki, polisi walienda nyumbani alikokuwa akiishi baba yake na kumkamata.
Shahidi wa kwanza, Kurwa Julius ambaye ni mjomba wa mtoto huyo, alidai kujulishwa na mtoto huyo kuwa baba yake (mrufani) alimuua mama yake kwa kumkata na sime kichwani na kumnyonga.
Julius alidai alijua dada yake (marehemu) na mtoto wake walikwenda kumtembelea baba yake na kuwa shahidi wa tano alimweleza kuwa alimuona mrufani akimshambulia mama yake.
Shahidi wa pili, Joshua Waryoba, alidai kuwa mwili wa marehemu ulikutwa kando ya Mto Mara kwenye lango la Ziwa Victoria.
Katika utetezi wake, mrufani alikana kuhusika na kifo cha aliyekuwa mke wake na kudai alipokea taarifa za kifo hicho siku alipokamatwa na kukana kuwa alikamatwa mbele ya shahidi wa tano na kudai kesi dhidi yake ilikuwa ya kutengenezwa.
Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili ilimkuta na hatia na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Katika rufaa hiyo, mrufani aliwakilishwa na Wakili Daud Mahemba huku Jamhuri ikiwakilishwa na mawakili wawili wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Madikenya.
Katika rufaa hiyo, mrufani huyo alikuwa na sababu tatu za kukata rufaa ambazo ni upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha kesi dhidi yake bila kuacha shaka yoyote, kwani hukumu yake ilitokana na ushahidi dhaifu, usio thabiti, wa ajabu na usioaminika.
Nyingine ni kesi ya utetezi haikuzingatiwa na mahakama na tatu ni mrufani hakutambuliwa na shahidi wa tano katika eneo la uhalifu.
Jaji amesema kuhusu hoja ya utambuzi wa mrufani eneo la tukio na kukagua kumbukumbu ya rufaa kwa makini suala la uamuzi wao ni kama mrufani alitambuliwa ipasavyo na shahidi wa tano ambaye kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka minne na ndiye shahidi pekee anayedaiwa kushuhudia tukio hilo.
Amesema ushahidi wa utambuzi wa mrufani eneo la tukio ulioshambuliwa na mrufani kutokana na umri wake na kuwa sheria imesuluhisha kuhusu uwezo wa shahidi, haibagui mtu yeyote kwa misingi ya umri bali kinachotakiwa ni uwezo wa shahidi katika kuelewa maswali anayoulizwa na kutoa majibu yenye maana.
Jaji huyo alielekeza kifungu cha 127 (1) cha Sheria ya Ushahidi, kinazungumzia suala hilo na kuwa umri wa shahidi wa tano usingeweza kumzuia kutoa ushahidi mbele ya mahakama, isipokuwa mahakama ikiona hakuwa na uwezo wa kuelewa maswali aliyoulizwa na kutoa majibu.
“Tunafahamu msimamo ulioamuliwa, kwamba uaminifu wa shahidi ni bora kutathminiwa na mahakama ya mwanzo ambayo ina fursa ya kusikiliza na kutazama shahidi anapotoa ushahidi na wakati wa kukata rufaa, kama ilivyo katika kesi ya sasa, tunatathmini ulinganifu wa ushahidi wa shahidi na tunauzingatia kuhusiana na ushahidi wa mashahidi wengine akiwemo mshtakiwa,” amesema.
Jaji Levira amesema katika kesi hiyo, mahakama ilitegemea zaidi ushahidi wa shahidi wa tano na kuwa kama siyo ushahidi wa shahidi wa tano, mrufani asingekamatwa, kufunguliwa mashtaka na kutiwa hatiani kwa mauaji.
Amesema wakiwa kama Mahakama ya Rufaa ya kwanza katika kesi hii kwa hivyo, wanayo fursa ya kutathmini upya ushahidi kwenye kumbukumbu.
“Katika tathmini yetu ya ushahidi wa shahidi wa tano, tunakubaliana mazingira hayaonyeshi kwamba shahidi wa tano alimtambua mrufani ipasavyo katika eneo la uhalifu, tunasema hivyo kwa sababu alisema hawezi kujua mshambuliaji kama mnene au mwembamba.”
Jaji Levira amesema hiyo inathibitisha kwamba shahidi wa tano hakumuona vizuri mtu aliyeingia kwenye chumba hicho na kumshambulia mama yake.
Jaji Levira amesema baada ya kupata matokeo hayo hawana sababu ya kuamua masuala mengine na kuwa ushahidi wa utambuzi wa mrufani eneo la tukio haukutosha kuthibitisha hukumu ya mrufani, hivyo kesi hiyo haikuthibitishwa na kuruhusu rufaa hiyo na kuamua mrufani aachiliwe huru mara moja.