Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amesema malezi na mafunzo wanayopata wanafunzi shuleni, hasa yanayosisitiza nidhamu na uwajibikaji, ni msingi muhimu katika kujenga taifa imara lenye uzalendo.
Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali kuendelea kuiombea Tanzania ili iendelee kuwa na amani na kuepuka athari za watu wanaotaka kuingiza nchi katika vurugu.
Balozi Nchimbi aliyasema hayo wakati wa kikao cha umoja wa wanafunzi waliosoma Shule ya Sekondari ya Uru Seminari, kilichofanyika Moshi, mkoani Kilimanjaro, baada ya ibada na mazishi ya aliyewahi kuwa Baba Gombera wa seminari hiyo, Padri Canute Mkwe Shirima AJ, mnamo Machi 20, 2025.
“Hakuna aliyesoma Uru Seminari asiyetambua mchango wa kipekee wa Padri Shirima. Tulifundishwa nidhamu, uwajibikaji, bidii kazini, na umuhimu wa kufuatilia mambo kwa umakini. Mafundisho hayo yametufanya kuwa watumishi bora katika nyanja mbalimbali za maisha,” alisema Balozi Nchimbi.
Aliongeza kuwa malezi ya walimu yana mchango mkubwa katika kujenga jamii yenye maadili na uzalendo, akisisitiza kuwa Taifa linapaswa kuthamini juhudi za walimu katika kujenga kizazi chenye maadili.
Katika kuendeleza maadili na mshikamano wa kitaifa, Balozi Nchimbi aliwasihi viongozi wa dini waendelee kuliombea Taifa na viongozi wake ili Tanzania iendelee kuwa nchi yenye utulivu.
“Nawaomba viongozi wa dini muendelee kuikabidhi nchi yetu kwa Mungu. Tuendelee kuiombea Tanzania, viongozi wake wa Serikali, CCM, na hata wa upinzani, ili Mungu aendelee kutuongoza. Kuna watu wenye nia ya kusababisha vurugu, hivyo ni muhimu sana tukaendelea kuilinda amani yetu,” alisema.
Aidha, alitoa pongezi kwa umoja wa wanafunzi waliosoma Uru Seminari kwa mshikamano waliouonyesha katika msiba wa Padri Canute, akiwahimiza kuendeleza umoja huo kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.