Licha ya kutopata muda mwingi wa kucheza katika kikosi cha Yanga, kiungo mshambuliaji Clatous Chama na mshambuliaji Kennedy Musonda wameitwa katika kikosi cha Zambia kwa ajili ya mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Urusi, Machi 25, 2025 jijini Moscow.
Kocha Avram Grant ameteua kikosi cha wachezaji 19 kwa ajili ya mchezo huo akiwajumuisha Musonda na Chama ambao wamekuwa hawana nafasi katika kikosi cha kwanza cha Yanga.
Ni kikosi kinachoundwa na kundi kubwa la wachezaji wanaocheza ligi ya Zambia huku kikiwa na wachezaji tisa wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi hiyo wakiwemo Musonda na Chama.
Kwa timu za Zambia, Zanaco ndio imeongoza kutoa idadi kubwa ya wachezaji katika kikosi hicho kilichotangazwa na Grant ambapo ina nyota watatu na inayofuatia ni Zesco United yenye wachezaji wawili.
Kikosi hicho kinaundwa na makipa Toaster Nsabata, Charles Kalumba na Victor Chabu huku mabeki wakiwa ni Gift Mphande, Benedict Chepeshi, Kabaso Chongo, Dominic Chanda na Kebson Kamanga.
Viungo wanaounda kikosi hicho ni Miguel Chaiwa, Dominic Kanga, Wilson Chisala, Kelvin Kapumbu, Emmanuel Banda, Kings Kangwa na Clatous Chama na washambuliaji ni Edward Chilufya, Songa Chipyoka, Kennedy Musonda na Joseph Banda.
Hata hivyo wakati Chama na Musonda wakijumuishwa katika kikosi cha Chipolopolo, winga ambaye amekuwa hapati nafasi ya kucheza katika kikosi cha Simba, Joshua Mutale ametoswa.
Huu ni muendelezo wa Zambia kumtosa Mutale ambaye kiwango chake kimeonekana kushindwa kulishawishi benchi la ufundi la Simba kumpa nafasi ya kucheza mara kwa mara kikosini