Marekani. Marekani imeendelea kushuhudia wimbi la uharibifu wa mali za kampuni ya Tesla, ikiwa ni pamoja na magari na vituo vyake, sababu ikitajwa kuwa ni hasira dhidi ya Elon Musk ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa Tesla na mkuu wa Idara ya Ufanisi wa Serikali (Doge).
Matukio haya ya hivi karibuni yamezusha taharuki miongoni mwa wamiliki wa magari ya Tesla na kuibua mjadala wa kitaifa kuhusu vurugu zinazolenga kampuni hiyo.
Machi 18, 2025, katika mji wa Las Vegas, Nevada, magari matano ya Tesla yaliharibiwa kwa moto na risasi katika moja ya vituo vya Tesla.
Polisi wa eneo hilo pamoja na Shirika la ujasusi la FBI, wameanzisha uchunguzi, lakini hakuna mshukiwa aliyekamatwa.
Hii ilifuatia tukio la Machi 17 huko Kansas City, Missouri, ambapo magari mawili ya Tesla yalichomwa moto, na kesi ya Machi 11 huko Dedham, Massachusetts, ambapo magari matatu yalipakwa rangi na matairi yake kuchomwa.
Mapema mwezi huu, Machi 7, kituo cha kuchaji Tesla huko South Carolina kilishambuliwa kwa mabomu ya moto, na mshukiwa, Daniel Clarke-Pounder (24), alikamatwa na kushtakiwa kwa uhalifu wa kuchoma mali.
Matukio hayo kwa sehemu kubwa yanahusishwa na jukumu la Elon Musk katika Doge, ambapo amepunguza wafanyakazi wengi wa Serikali na bajeti za mifuko ya umma.
Wachambuzi wa mambo wanadai kuwa hatua hizo za Musk serikalini zimewakera baadhi ya Wamarekani, wengi wao wakiwa wafanyakazi wa serikali waliopoteza kazi au wafuasi wao, na sasa wameamua kulenga Tesla kama njia ya kulipiza kisasi.
Tangu Musk apewa nafasi hiyo na Rais Trump, kumekuwa na wimbi la uharibifu, kutoka kupakwa rangi za maandishi kwenye magari hadi matumizi ya risasi na moto, yote yakionekana kama maandamano dhidi ya sera zake.
Wakili Mkuu wa Marekani, Pam Bondi, ameyataja matukio haya kama “ugaidi wa ndani” na kuahidi kuwafikisha wahusika mbele ya sheria, ikiwa ni pamoja na adhabu za miaka mitano ya kifungo kwa wengine.
FBI imechukua hatua za kuchunguza, hasa tukio la Las Vegas, ambalo wanaamini lilifanywa na mtu mmoja aliyejificha usoni.
Wamiliki wa magari ya Tesla wameelezea hofu yao.
Mmoja wao alisema, “Inatia woga kuona magari yetu yakilengwa kwa sababu tu ya siasa za Musk. Hatukutarajia hili.”
Kwa upande mwingine, waandamanaji wanaona Tesla kama chombo cha Musk cha kuharibu serikali, wakisema, “Tunapaswa kupaza sauti zetu dhidi ya hiki.”
Hii inaonyesha mgawanyiko wa maoni, wamiliki wakihofia usalama wao, huku wapinzani wakitumia uharibifu kama silaha ya kisiasa.