Wiki iliyopita tuliona matatizo ya kiafya yanayoweza kujitokeza wakati wa kufunga, yaani kujinyima kula kwa zaidi ya saa 16. Leo tutaona vitu vya kufanya kujikinga matatizo ya kiafya kutokana na kufunga.
Kunywa maji: Kunywa maji mara kadhaa usiku kucha angalau glasi 10 baada ya kufungua mpaka kulala. Kunywa hata kama hujisikii kiu, hali ya kiu ni ishara kwamba mwili tayari una upungufu wa maji.
Chagua maji ambayo hayana kafeini, kwa sababu vinywaji vyenye kafeini vinaweza kupunguza maji mwilini kwa sababu huchochea mkojo zaidi.
Kuwa mwangalifu kutokunywa maji mengi kwa mkupuo, kwani kunaweza kupunguza chumvi chumvi za mwili wako. Pendelea maji ya uvuguvugu, kwani yananyonywa kirahisi na mwili.
Lishe mchanganyiko: Kula vyakula mbalimbali wakati wa jioni, ikiwamo juisi za matunda, kwani husaidia kukurudishia maji na madini mbalimbali. Mwili wako unahitaji lishe bora ili kufidia vitu vilivyokosekana wakati wa kufunga.
Tumia nafaka zisizokubolewa, mboga mboga, matunda, protini isiyo na mafuta, mafuta yenye afya kutoka kwenye mimea, kama mafuta ya alizeti.
Mfano nafaka zisizokobolewa kama dona, mkate wa ata, mchele wa kahawia, vinawafaa zaidi wale wanaofunga watu wazima wenye uzito uliokithiri au unene.
Muhimu pia kufungua mlo na supu au uji mwepesi au mtori. Epuka kutumia vyakula vyenye viungo vingi au tindikali nyingi, sukari, mafuta mengi na chumvi nyingi.
Kula mlo wa kufungua kwa kiasi: Kula mlo wa kiasi kunakupa nguvu zaidi kuliko kula kiasi kikubwa kwa wakati mmoja. Huhitaji kula kupita kiasi, kwani unauchosha mwili.
Endelea kufanya kazi za kimwili: Ingawa kufunga kunaweza kuchosha kimwili, jaribu kuepuka kulala saa nyingi, badala yake shughulisha mwili kwa kazi za hapa na pale.
Ikiwa kwa kawaida unafanya mazoezi asubuhi, angalia jinsi mwili wako unavyohisi ukibadilisha mazoezi hadi jioni baada ya kufungua.
Mazoezi ya nguvu au kazi ngumu siyo nzuri wakati wa mchana, kwa sababu unaweza kupoteza maji haraka, hasa wale ambao wako katika maeneo yenye joto.Inashauriwa kufanya matembezi mafupi rahisi, kwani yanaweza kusaidia sana kuweka nguvu zako wakati wa mchana.
Tafuta kile kinachofaa ili kupumzika na kulala:
Wapo ambao pindi wanapokula tu hujisikia kulala. Vizuri ulaji wako kila wakati uendane na ratiba ya kulala usiku na kuamka kula tena kwa wale wanaokula daku.
Hakikisha mlo wa daku uwe mwepesi na rahisi kusagwa na kunyonywa. Kumbuka usiku mwili huhitaji kulala zaidi ili kujisahihisha na kujijenga kuliko kufanya kazi ngumu ya kusaga mlo.
Jenga hisia kuboresha afya ya akili: Jivunie kuwa kufunga ni furaha na si kujitesa. Huu ni mwezi wa furaha zaidi katika mwaka, furahia milo ya pamoja na wengine, fanya mazoezi mepesi ya kutembea, kuwa mvumilivu kwako binafsi na wengine.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kufunga na kuchangamana na wanajamii wengine kunaboresha afya ya akili zaidi.
Iwapo una kikwazo katika kufunga ni vyema kuwaona viongozi wa dini wakuelimishe au waone watoa huduma za afya wakushauri kuhusu lishe na kufunga.