Jeshi la Serikali Sudan lafanikiwa kuikomboa Ikulu, waasi wafurushwa

Darfur. Jeshi la Sudan limefanikiwa kuirejesha Ikulu ya taifa hilo iliyopo mji mkuu, Khartoum, nchini Sudan baada ya mapigano makali dhidi ya kundi la wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF) yaliyodumu kwa takriban miaka miwili iliyopita.

Kundi la RSF linaongozwa na Jenerali Mohammed Hamdan Dagalo ambaye alifanya uvamizi na kutaka kuipindua Serikali ya Rais wa mpito, Luteni Jenerali Abdel-Fattah Burhan.

Taarifa iliyotolewa na vyanzo vya habari nchini humo, vimeripoti kupitia Ofisa Habari wa Jeshi la Sudan, Nabil Abdallah, kwamba wamefanikiwa kuudhibiti mji huo na kudhibiti majengo mengine muhimu katikati mwa Khartoum huku wakifanikiwa kukamata vifaa na silaha nyingi za wapiganaji hao.

Msemaji huyo wa jeshi la nchi hiyo alieleza kuwa jeshi hilo litaendelea kusonga mbele katika nyanja zote hadi litakapofanikiwa kuyarejesha maeneo yote yanayokaliwa na RSF.

Jengo hilo la kimkakati lililotekwa na RSF haraka limeonekana kuwa magofu, ambapo wanajeshi hao wameonekana ndani ya jengo hilo wakiwa wamebeba silaha ikiwemo bunduki na mabomu huku wakiimba ‘Mwenyezi Mungu ndiye mkuu zaidi’.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari wa Sudan, Khaled al-Aiser, ameandika katika akaunti yake ya mtandao wa X (zamani Twitter), kuwa jeshi limechukua tena udhibiti wa Ikulu na kuahidi kuwa bendera itapandishwa sambamba na kuendeleza mapambano hadi watakapofanikiwa kuvifutilia mbali vikundi vya waasi nchini humo.

Licha ya kundi la RSF kuondolewa katika mji wa Khartoum, bado halijakiri kushindwa kwani Alhamisi wiki hii lilidai kuwa huenda lisisitishe mapigano kwani RSF na washirika wake bado wameonyesha mgomo katika kuukabili mji wa al-Maliha Sudan ambao pia ni mji wa kimkakati wa jangwa huko Kaskazini mwa Darfur.

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (Unicef) amesema mzozo huo umesababisha vita hivyo vilivyowafanya mamilioni ya watu kuyakimbia makazi yao katika jitihada za kujinusuru huku njaa ikikumba sehemu mbalimbali za nchi na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 28,000.

Ikumbukwe kuwa Ikulu ya ‘Republican’ ndiyo ilikuwa makao makuu ya utawala wakati wa ukoloni wa Uingereza nchini Sudan. Pia, iliona baadhi ya bendera za kwanza huru za Sudan zikipandishwa juu ya nchi mwaka 1956.

Pia, ilikuwa Ofisi Kuu ya Rais wa Sudan na maofisa wengine wakuu.

Jeshi la Sudan kwa muda mrefu limekuwa likilenga jumba hilo na viwanja vyake, wakishambulia kwa makombora na kufyatua risasi kwenye boma hilo bila mafanikio hadi jana walipofanikiwa kuingia na kuwafurusha wapiganaji wa RSF.

Sudan, taifa lililo Kaskazini-Mashariki mwa Afrika, halijapata utulivu tangu ghasia za wananchi kulazimisha kuondolewa madarakani kwa Rais wa muda mrefu Omar al-Bashir mwaka 2019.

Uongozi wa Omar al-Bashir ulikoma baada ya Burhan na Dagalo kuongoza mapinduzi ya kijeshi mwaka wa 2021, hata hivyo, wawili hao walitofautiana na kuanza kupigana wenyewe huku Burhan akichukua udhibiti wa Serikali ya nchi hiyo.

Wawili hao walimng’oa madarakani al-Bashir, aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) akituhumiwa kutekeleza mauaji ya halaiki miaka ya 2000 katika eneo la Darfur magharibi na Janjaweed nchini humo.

Imeandikwa na Timothy Lugoye kwa msaasa wa Mashirika.

Related Posts