Kibu Dennis Avunja Ukame wa Mabao Baada ya Siku 494 – Global Publishers


KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Kibu Dennis aliyeyusha siku 494 ambazo ni wiki 70 bila kufunga bao kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ni namba nne kwa ubora Afrika.

Nyota huyo ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Fadlu Davids ni kiungo mwenye nguvu na jina lake lipo kwenye orodha ya nyota walioitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo dhidi ya timu ya taifa ya Morocco.

Huo ni mchezo kwa ajili ya kuwania kufuzu Kombe la dunia 2026 chini ya Kocha Mkuu, Hemed Suleiman, (Morocco) ambapo kikosi hicho kinajumuisha wachezaji 24 watakaokuwa na kazi ya kuipambania nembo ya taifa ya Tanzania.

Rekodi zinaonyesha kuwa mara ya mwisho Kibu kufunga ilikuwa Novemba 5 2023 ilikuwa dhidi ya Yanga, mchezo huo wa Kariakoo Dabi ulichezwa Uwanja wa Mkapa na baada ya dakika 90 ubao ukasoma Simba 1-5 Yanga, Simba waliyeyusha pointi tatu mazima ndani ya dakika 90 kwenye mchezo huo.

Hivyo Novemba 5 2024 Kibu anayevaa jezi namba 38 ndani ya kikosi cha Simba alitimiza mwaka bila kufunga bao ndani ya ligi licha ya nafasi ambazo alikuwa akipata kuanza kikosi cha kwanza na wakati mwingine alikuwa akianzia benchi.

Ule usemi wa usimkatie mtu tamaa ulijibu kwa kuwa siku ambayo wengi hawakutarajia iliwadia na mwamba akafungua akaunti yake ya mabao kwa msimu wa 2024/25 kwa kufunga mabao mawili ndani ya uwanja.
Ilikuwa ni Machi 14 2025 kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Dodoma Jiji, Uwanja wa KMC Complex nyota huyo aliandika rekodi yake kwa kufunga na kutoa pasi katika mchezo huo.

Baada ya kufunga mabao mawili na kutoa pasi mbili za mabao ilimfanya ahusike kwenye mabao manne kati ya sita yaliyofungwa na timu hiyo dhidi ya Dodoma Jiji walipokomba pointi tatu mazima.

Kibu alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo ambapo ilikuwa ni tuzo yake ya kwanza kuibeba akiwa na uzi wa Simba ndani ya msimu wa 2024/25 kutoka ligi namba nne kwa ubora Afrika.

Anayo mabao mawili kibindoni akiwa amecheza jumla ya mechi 16 akikomba dakika 1,110 akiwa na pasi 3 za mabao kahusika kwenye mabao matano kati ya 52 yaliyofungwa na timu hiyo.

Kibu ana wastani wa kuwa na hatari kila baada ya dakika 222 akiwa uwanjani na Simba ni mechi 22 ilishuka ndani ya msimu wa 2024/25 akiwa kakosekana kwenye mechi sita.
Kwenye msimamo Simba ni namba mbili baada ya mechi 22 ambazo ni dakika 1,980 kibindoni imekusanya jumla ya pointi 57 na vinara ni Yanga wenye pointi 58.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM. Kuna kazi mpya inaandaliwa inaitwa Moyo Wangu Unavuja Damu usipange kukosa.

Related Posts