Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amefunguka namna alivyokomaa Angola hadi akahakikisha ameshiriki mkutano wa siku tatu ambao ulikumbwa sitofahamu baada ya wahudhuriaji kutoka nje kuzuiliwa uwanja wa ndege.
Katika mazungumzo yake na Mwananchi Lissu alieleza sababu za yeye kuendelea kusalia nchini Angola, licha ya baadhi ya viongozi wengine akiwemo Makamu wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Othman Masoud na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu kwa pamoja walizuiwa na mamlaka za taifa hilo kuingia nchini humo, Machi 13,2025 katika Uwanja wa Ndege wa Quatro de Fevereiro jijini Luanda.
Siyo hao pekee, bali hata viongozi wengine mashuhuri wakiwemo marais wastaafu kutoka Botswana na Colombia, Waziri Mkuu mstaafu wa Lesotho na baadhi ya wakuu wa vyama vya siasa kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika walikumbwa na kadhia hiyo.
Kutokana na kadhia ujumbe wa Othman na Semu ulilazimika kurejea Tanzania kwa nyakati tofauti huku wakilaani hatua ya Serikali ya Angola kuwazuia washiriki mazungumzo ya Jukwaa la Demokrasia Afrika (PAD). Mazungumzo yaliyoandaliwa na Taasisi ya The Brenthurst Foundation.
Katika maelezo yake, Lissu aliyerejea Tanzania, akitokea Angola usiku wa kuamkia leo Ijumaa, amesema “Nilishiriki mkutano, nilikomaa, sikutumia njia zozote bali nilikomaa tu kwa kuwaambia watueleze kwa nini wanatukataza kuingia Angola, kwa kosa gani?
“Niliwaeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Angola tangu miaka hiyo, kisha nikawauliza hivi nyie kweli wa kunizuia nisiingie Angola? Ebu acheni utani wenu … Oohh … Ooh sijui nini tukakomaa mwisho wa siku wakaturuhusu.
“Nilikaa uwanja wa ndege kwa saa tisa kuanzia saa sita mchana hadi saa nne usiku, baadaye wakaturuhusu, lakini hakufanikiwa kwenda Benguela ambako mkutano ulipangwa kufanyika, badala yake tulifanyia jijini Luanda,” amesema Lissu.
Hata hivyo, Lissu anasema mkutano huo wa siku tatu ulikwenda vizuri, ingawa ungefanyika Benguela ungekuwa mzuri zaidi kwa sababu maandalizi makubwa yalifanyika huko ikiwemo mkutano mkubwa wa hadhara ulioandaliwa.
Aidha Lissu alisema yupo ‘fiti’ kushiriki kampeni ya ‘No Reforms No Election’ itakayofanya mikutano nchi nzima kwa siku 48.
Kampeni ya ‘Bila mabadiliko, Hakuna uchaguzi’ itazinduliwa Machi 23, 2025 katika Kanda ya Nyasa yenye mikoa ya Iringa, Mbeya, Rukwa, Songwe na Njombe. Kisha kuanzia Aprili 4 hadi 10 kampeni hiyo itaelekea Kanda ya Kusini (Ruvuma, Mtwara na Lindi)
Lengo la kampeni hiyo ni kupeleka elimu kwa wananchi ya kuishinikiza Serikali kufanya mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi, vinginevyo uchaguzi usifanyike.
Uamuzi huo ‘No Reforms, No Election’ ulipitishwa Desemba 2024 na Kamati Kuu ya chama hicho, kabla ya msimamo huo kuthibitishwa na Mkutano Mkuu Januari 21, 2025.
Hata hivyo, Machi 18, 2025 viongozi waandamizi wa Chadema, wakiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika waliitikia wito wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, iliyowataka kufafanua ajenda hiyo, kwa muktadha wa Sheria ya Vyama vya Siasa.
Tundu Lissu amesema, “Nimesharudi (kutoka Angola), tarehe 23, tutakuwa Mbeya. Sina shida yote nipo fiti, tutafanya kwa kadri Mungu atakavyotuwezesha,” amesema Lissu.
Katika ziara hiyo, Lissu ataambatana na Makamu Mwenyekiti (Bara) John Heche, manaibu makatibu wakuu na wajumbe wa kamati kuu. Viongozi hao watakuwa na jukumu la kuelimisha umma kuhusu ajenda ya ‘Hakuna mabadiliko, Hakuna uchaguzi’.
Machi 19,2025 Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), aliwaambia wanahabari kuwa, “Baada ya mkutano wa Mbeya mjini tutakuwa na timu mbili, ya kwanza itakayongozwa na Lissu, nyingine Heche katika mikoa na majimbo ya Kanda ya Nyasa.
“Tukimaliza timu zote zitakutana Iringa mjini Machi 29, kuhitimisha ziara ya Kanda ya Nyasa,” amesema Golugwa.