Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesema wanapozungumza msimamo wa chama wa ‘No reforms No Election’ wanategemea kauli hiyo iungwe mkono zaidi Zanzibar kwa sababu ndiyo waathirika wakubwa wa masuala ya uchaguzi.
Lissu ametoa kauli hiyo leo Machi 21, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Kuu za chama hicho Unguja, ambapo amesema msimamo wa chama hicho si kususia uchaguzi bali ni kuuzuia kwa kuwaeleza wananchi madhara yatakayotokea iwapo ukifanyika kukiwa na mifumo ileile.
“Tunapuzungumza ‘No reform, No election’, sio kwamba tunasusia uchaguzi, lakini tunazuia uchaguzi na kauli hii tunategemea isikike zaidi hapa Zanzibar kwa sababu ambazo zipo wazi kutokana na madhira ambayo yamekuwa yakitokea katika uchaguzi,” amesema.
“Matatizo ya uchaguzi, yamekuwa mengi zaidi, makubwa zaidi na mabaya zaidi kwa Zanzibar kuliko Tanganyika, kama kumbukumbu zinavyotuonyesha upinzani mkubwa umekuwa Zanzibar kuliko Tanganyika, tangu mfumo wa vyama vingi unaanzishwa mwaka 1992, tayari kulikuwa na upinzani Zanzibar,” amesema.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Tundu Lissu akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho Unguja. Picha na Jesse Mikofu
Kwa mujibu wa Lissu, Zanzibar ndio sehemu ambayo kumeshuhudiwa ukandamizaji, mauaji ya watu wasio na hatia wakati chaguzi zinapofanyika.
Amesema wanapozungumza kwamba kama hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi, halafu kuna watu wanasema wao watashiriki uchaguzi kwa namna yoyote ilivyo bila kuwapo mabadiliko yoyote, hatua hiyo inashangaza kwa kuwa yanapozungumzwa matatizo yanayohusina na uchaguzi chimbuko lake ni Zanzibar.
“Tunapozungumzia matatizo ya uchaguzi na changamoto zote, mfano wa kwanza ni Zanzibar, kwa hiyo kama kuna sehemu inahitaji mabadiliko makubwa ya uchaguzi basi ni katika kisiwa hicho,” amesema.
Kwa mujibu wa Lissu, kazi ya kuleta mabadiliko katika taifa hili kwa pande zote mbili ikiachiwa Chadema peke yao hawataiweza, hivyo kila mmoja anayeumizwa na mambo hayo anapaswa kuunga mkono ili kwa pamoja waweze kushinikiza na kufanyika mabadiliko ya kimifumo ili kusaidia maendeleo ya taifa.
“Nchii hii ni kubwa sana, inahitaji mikono na baraka za wengi, kwa hiyo ndugu zangu tushikamane kuyapigania haya tunayoyapigania,” amesema.
Akizungumza kuhusu Muungano, Lissu amesema msimamo wa chama hicho ni uleule kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unakandamiza upande mmoja na kutoa nafuu kwa upande mwingine, kwa hiyo ipo haja kila upande ukawa na mamlaka yake kamili.
“Huu muungano haujatenda haki, kwa miaka yote Zanzibar imekuwa ikivalishwa koti linaloibana, haya sio maneno yangu tu, yalianza tangu mwaka 1983 kwa Aboud Jumbe na Maalim Seif amekuwa akiimba jambo hili,” amesema.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Mzee amesisitiza kuwa “No reform, No election” inahitajika zaidi Zanzibar kuliko Tanzania Bara.
Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche amesema bahari ni rasilimali tosha ambayo iwapo ikitumika vema inaweza kuendesha uchumi wa kisiwa hicho.
“Bado suala la uchumi wa buluu halijaeleweka kwa wananchi wengi kwa hiyo ipo haja ya kufafanua na kutumia rasilimali za bahari kwa uchumi wa Zanzibar,” amesema.