UKIANGALIA takwimu za makipa wenye cleansheet nyingi kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu, Moussa Camara wa Simba anaongoza akiwa nazo 15, akifuatiwa na Djigui Diarra wa Yanga mwenye 11.
Makipa hao ambao wote ni raia wa kigeni, Camara akitokea Guinea na Diarra nchini Mali, wamekuwa wakicheza kikosi cha kwanza kwenye klabu zao sambamba na timu za taifa.
Mastaa wa zamani wa Simba na Yanga, wamesema ujio wa Camara msimu huu umeibua ushindani dhidi ya Diarra. Lakini Jean Baleke ametamka moja kwa moja kwamba Camara ni namba moja kwake.
Camara ambaye anacheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu huu, amedaka katika mechi 20 kwa dakika 1,800 akiruhusu mabao manane katika michezo tano dhidi ya Coastal Union (mabao mawili), Yanga (bao moja), Fountain Gate (bao moja), Azam (mabao mawili) na Kagera Sugar (mabao mawili).
“Diarra ni kipa mzuri, muda aliocheza katika Ligi ya Tanzania ameonyesha na kuthibitisha ubora wake, hivyo kupewa changamoto ya ushindani na Camara ambaye anacheza msimu wake wa kwanza na bado ana kazi ya kufanya kuendeleza alichokianza siyo kitu kibaya katika soka,” alisema Baleke ambaye wakati anacheza Simba alifunga jumla ya mabao 16 akiingia dirisha dogo 2022/23 na kuondoka dirisha dogo la 2023/24, kisha akiwa Yanga iliyomtema baada ya kumsajili 2024/25 aliifungia bao moja.
Kiungo mshambuliaji wa Tabora United, Offen Chikola ambaye amefunga mabao saba katika Ligi Kuu huku mawili akimtungua Diarra, alisema: “Diarra na Camara wana ushindani wa kuonyeshana ubora wao wakiwa golini, mfano sisi washambuliaji lazima utumie akili kubwa kuwafunga.”
Huu ni msimu wa nne kwa Diarra ndani ya Ligi Kuu Bara tangu alipojiunga na Yanga 2021 akitokea Stade Malien, kadaka mechi 16 yuko nyuma ya Camara kwa mechi nne, kacheza dakika 1440, kafungwa mabao sita, ana clean sheets 11.
Kipa wa zamani wa Simba, Yanga na Stars, Ivo Mapunda amesema kitendo cha kutajwa Diarra na Camara kinaonyesha namna ushindani wao ulivyo mkubwa na msaada wao katika klabu wanazozitumikia.
“Diarra kathibitisha ubora wake tangu alipojiunga na Yanga 2021 hadi 2025, ila ukiona mashabiki wanakuzungumzia ujue una kitu kizuri unakifanya ndicho ninachokiona kwa Camara ambaye huu ni msimu wake wa kwanza, hivyo kaleta ushindani kwa Diarra, timu hizo zinapocheza wakiamini eneo la makipa lipo salama,” alisema Mapunda.
Kipa wa zamani wa Simba na Stars, Idd Pazi ‘Father’ alisema kuna mambo yanafanana kwa Diarra na Camara kama kujiamini kupita kiasi, kitu kinachoweza kikawasaidia kuwafanya wapinzani wao wawahofie ama kuwagharimu kama ilivyotokea kwa baadhi ya michezo yao ya Ligi Kuu.
Alisema Yanga iliposhinda mabao 6-1 dhidi ya KenGold bao alilofungwa Diarra alitoka nje ya sita akashindwa kurudi nyuma kwa haraka, vivyo hivyo kwa Camara Simba ilipotoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Coastal Union alitoka eneo lake wakatumia udhaifu huo kumfunga, unaweza ukaona wana viwango vinavyofanana kwa ubora na udhaifu wao.
“Ujio wa Camara umeibua ushindani dhidi ya Diarra ambaye tangu kajiunga Yanga kathibitisha kiwango chake kuwa bora, ingawa ukitazama kwa upande wa makosa yapo mambo waliyofanana,” alisema Pazi.