Mchengerwa awaka malori kupita mwendokasi Mbagala, ampa ujumbe RC

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amekosoa uamuzi wa kuruhusu magari kupita kwenye barabara za mabasi yaendayo haraka (BRT) bila kibali cha wizara hiyo.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mikataba ya awamu ya pili ya Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP II), leo Ijumaa Machi 21, 2025, Mchengerwa amesisitiza kuwa barabara hizo ziko chini ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), ambao upo chini ya Ofisi ya Rais Tamisemi.

“Wakati fulani mlitoa maelekezo ya kuruhusu watu kupita kwenye barabara za mwendokasi, mkasahau kuwa barabara hizo siyo za kwenu. Sasa barabara ya mwendokasi ya Mbagala imeanza kuharibika kwa sababu ya malori makubwa ya tani 30 hadi 40 yanayokatiza katikati. Madhara yake ni makubwa na miradi yote ya ujenzi wa barabara inaweza kuathirika,” amesema Waziri Mchengerwa.

Aidha, amesema Serikali itapitia upya utaratibu wa mgao wa mapato ya ndani ili kuongeza bajeti ya barabara, kwa lengo la kuwezesha Tarura kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. 

“Hatuwezi kuendelea kuwa na mgao wa asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya barabara, lazima tuhakikishe Tarura ina uwezo wa kufanya kazi saa 24 ili kuhakikisha barabara zinajengwa kwa viwango na kwa wakati,” ameongeza. 

Katika hafla hiyo, Waziri Mchengerwa alishuhudia utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 84.4 katika Halmashauri mbalimbali za Jiji la Dar es Salaam chini ya DMDP TWO. 

Endelea kufuatilia Mwananchi

Related Posts