Geita. Mfanyabiashara wa pembejeo za kilimo na mifugo katika mji mdogo wa Katoro uliopo Wilaya ya Geita mkoani Geita, Tatu Kimori (46) amepotea katika mazingira ya kutatanisha kwa siku 19.
Mfanyabiashara huyo anadaiwa kupotea kuanzia Machi 2, 2025 baada ya kupigiwa simu na kuelezwa mzigo wake wa pembejeo alioagiza umekamatwa mpakani mwa Sirari na hivyo kutakiwa kuufuata.
Mume wa mwanamke huyo, Yohana Zacharia, ambaye naye ni mfanyabishara wa pembejeo, amesema baada ya mkewe kupata simu, alimjulisha na kuanza safari lakini baada ya kufika Sirari, simu yake haikupatikana na hadi sasa hajulikani alipo.
Zacharia amesema tayari ametoa taarifa polisi na kupewa RB namba GER/ GD/PE/48/2025.
Mwananchi limefika Ofisi ya Polisi Geita kujua hatua zilizochukuliwa, hata hivyo Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Adam Maro ameshauri mwandishi kuwasiliana na Polisi Kanda Maalumu ya Tarime Rorya.
Mwandishi amewasiliana kwa njia ya simu na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Mark Njera, hata hivyo amejibiwa kwa ujumbe mfupi wa maneno kwamba hana taarifa hizo.
Zacharia ambaye ni mume wa mfanyabiashara huyo, amedai Machi Mosi, 2025, mkewe aliondoka nyumbani na kwenda Nzega na kumpa dereva gari ili ampeleke na jioni dereva alimpigia simu akimueleza amerudi salama.
Amedai baada ya kupata simu ya dereva, aliwasiliana na mkewe akimtaka achukue kadi ya harusi nyumbani ili waungane kwenda kwenye sherehe lakini mkewe alidai amepigiwa simu kuwa mzigo alioagiza umekamatwa Sirari.
“Mke wangu aliniambia anafuatilia huo mzigo na nilimuuliza usiku ataendaje Sirari, lakini alidai anaenda na kwa kuwa huwa tunaagiza mizigo mara kwa mara, sikuwa na hofu na kesho yake asubuhi, aliniambia amefika Sirari salama na huo ndio ulikuwa mwisho wa kuwasiliana naye,” amesema Zacharia.
Amesema alitoka asubuhi ili akafungue duka na kumpigia simu mkewe ili kujua alikoweka ufunguo lakini simu haikupatikana siku nzima.
Amesema aliendelea kumtafuta kwa njia ya simu bila mafanikio na kuanza kutoa taarifa kwa ndugu lakini mkewe hakuwa amewasiliana na yeyote, jambo lililompa hofu.
“Tulipoona hapatikani na hajawasiliana na yeyote niliamua kuondoka hapa Katoro na ndugu mwingine, nikafika Sirari, nikaenda polisi upande wa Tanzania na Kenya na Mamlaka ya Mapato (TRA) ambako kote walidai hawajamuona na hakuna mzigo wanaoushikilia,” amesema Zacharia.
Zacharia ameiomba Serikali na Jeshi la Polisi kufuatilia ili ajue aliko mke wake na kama yuko salama.
Chacha Kimori ambaye ni kaka wa mwanamke huyo, amesema kama familia wana hofu kwa kuwa hawajui aliko ndugu yao na hawajui kama ametekwa au la.
Amesema wao kama familia kwa sasa tumaini lao liko kwa Serikali na polisi na wanaomba juhudi zaidi zifanyike ili ndugu yao apatikane.