Mrundi jela miezi mitatu kwa uongo, kuvunja sheria

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu raia wa Burundi, Alex William, kulipa faini ya Sh1 milioni au kwenda jela miezi mitatu baada ya kupatikana na hatia ya kuwepo nchini Tanzania bila kuwa na kibali pamoja  na kutoa taarifa za uongo ofisi za Uhamiaji.

Hukumu hiyo, imetolewa leo Machi 21, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankunga, baada ya mshtakiwa kukiri mashtaka yake aliposomewa mashtaka yake kwa mara ya kwanza.

Hata hivyo, mshtakiwa ameshindwa kulipa faini, hivyo ameenza maisha mapya gerezani.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mshtakiwa alisomewa mashtaka yake na Wakili wa Serikali Hadija Masoud,

Wakili Masoud alidai shtaka la kwanza, mshitakiwa anadaiwa Machi 4, 2025 alikutwa akiishi nchini Tanzania bila kuwa na kibali wilaya ya Temeke.

Shtaka la pili, inadaiwa siku hiyo mshitakiwa alikwenda ofisi za Uhamiaji Temeke, Dar es Salaam na kutoa taarifa za uongo kwa ofisa Uhamiaji aweze kupata kitambulisho cha Taifa.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, alikiri kutenda na Hakimu Gwantwa alimtia hatiani kama alivyoshitakiwa.

Hata hivyo, mahakama ilipompa nafasi ya kujitetea mshtakiwa huyo, aliomba apunguziwe adhabu kwa kuwa ni kosa lake kwanza na kwamba aliingia nchini kutafuta maisha.

“Mahakama imekutia hatiani kama ulivyoshtakiwa na hivyo, katika shtaka la kwanza la kuwepo nchini bila kibali, mahakama inakuhukumu kulipa faini Sh500,000 au kwenda jela miezi mitatu, shtaka la pili la kutoa taarifa za uongo, faini Sh500,000, au jela miezi mitatu” amesema hakimu Gwantwa.

Related Posts