Dar es Salaam. Wananchi wa mkoa wa Tabora wataepukana na changamoto ya umeme baada ya kuwashwa rasmi laini ya msongo wa kilovolti 132 yenye urefu wa kilomita 115.
Mradi ulianza Aprili 2024 na ulitegemewa kumalizika Juni 2025.
Mradi huo utasaidia kuchochea maendeleo katika Wilaya ya Urambo, Kaliua na Mkoa wa Tabora kwa ujumla.
Akizungumza leo Machi 20, 2025 mkoani Tabora katika shughuli ya kuwasha laini hiyo, Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme ( ETDCO), Sadock Mugendi amesema wategemee kupata umeme wa uhakika.
“Licha ya uhakika wa kupatikana kwa umeme pia mradi huu umetekelezwa na wataalamu wazawa, jambo ambalo limeonyesha tunaweza kutekeleza miradi ya umeme kwa wakati bila tatizo lolote,” amesema Mugendi.
Amesema wameshukuru kumaliza mradi huo kabla ya wakati ili wananchi waweze kupata umeme wa uhakika haraka iwezekanavyo.
Meneja wa Mradi wa Tabora – Katavi kwa upande wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Sospeter Oralo amesema mradi huo umegharimu Sh40 bilioni.
Amesema gharama ya laini yya Kilovolti 132 kutoka Tabora hadi Urambo ni Sh24 bilioni huku ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Urambo zimetumika Sh16 bilioni.