Mtazamo tofauti uzito kuzidi kwenye mizani

Dar es Salaam. Wamiliki wa malori, madereva na wadau wa usafirishaji wamezungumzia changamoto za mizani kutoa taarifa tofauti za uzito, huku ubovu na kutofanyiwa ukarabati wa mara kwa mara vikitajwa.

Hayo yameelezwa leo Machi 21, 2025 ikiwa ni siku moja baada ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, kuwasimamisha kazi watumishi waliokuwa zamu katika mizani kutoka Tunduma, Mkoa wa Songwe, hadi Vigwaza, Mkoa wa Pwani, kupisha uchunguzi.

Agizo hilo alilitoa baada ya kuunda timu ya wataalamu kuchunguza tuhuma zinazowagusa watumishi hao waliokuwa zamu Machi 13, 2025.

Hatua hiyo inatokana na kusambaa picha mjongeo kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha dereva aliyetambulika kwa jina moja la Pamela akilalamikia kunyanyaswa katika mzani wa Vigwaza.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Ulega alisema hatua hizo zimechukuliwa baada ya yeye kushauriana na menejimenti na wataalamu baada ya Pamela, aliyekuwa akiendesha gari la mzigo lenye tela, kulalamika kuhusu tabia na maneno ambayo yalijitokeza dhidi yake.

Pamela alilalamika kuhusu mizani ya Vigwaza kuonyesha amezidisha uzito ilhali alipita maeneo mengine kote na hilo halikuonekana.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Machi 21, 2025 Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Rahim Dosa, amesema wiki mbili zilizopita walijadili kuhusu ubovu wa mizani jijini Dodoma wakiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

“Alichofanya dereva yule kutoka mbele ya umma na kuzungumzia kero hiyo ya mizani hajawazungumzia madereva tu, bali katuwakilisha na sisi wamiliki kwa kuwa ni suala ambalo limekuwa likituumiza kwa muda mrefu,” amesema.

Kwa mtazamo wake, tatizo kubwa ni mizani kutofanyiwa ukarabati wa mara kwa mara na kuongezeka magari makubwa hivyo kutokuwa na uwiano sawa.

Amesema hatua ya kufanya uchunguzi ni nzuri kwa kuwa huenda kuna watumishi wanaotumia mwanya uliopo katika usimamizi kuihujumu Serikali.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Madogo na ya Kati (Tamstoa), Chuki Shabani amesema mizani za Iringa na Makambako ndizo zenye shida na kilio kwa mara kadhaa wamekifikisha serikalini.

“Haiwezekani mtu anatoka bandarini uzito wa mzigo  upo sawa, lakini akifika mizani ya Kwala anaambiwa umezidi, analipa faini, halafu akifika tena Mikese anaambiwa upo sawa, anajikuta alishaingia gharama ya kulipa faini kumbe hakuwa hata na kosa,” amesema.

Anashauri watumishi kwenye mizani wasiachwe muda mrefu wakazoea ofisi kwa kuwa huenda nao kwa namna moja au nyingine wanashiriki ili kujipatia fedha zisizo halali.

Mbali na hilo, amewataka madereva kuacha kubeba mizigo njiani isiyohusiana na walioagizwa, kwa kuwa wengine wamekuwa chanzo cha magari kuzidi uzito na mwisho wa siku anayeumia ni mmiliki kwa kulipishwa faini.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Malori Tanzania (Chawamata), Nuhu Mgodoka, amesema mara nyingi wamekuwa wakishughulikia kero hizo kwa kuwasiliana na viongozi wa mizani na hata kuzitembelea.

Mgodoka amesema kwa kuwa Serikali imeshachukua hatua za uchunguzi, wanaacha ifanye kazi yake na kuleta majibu.

Hata hivyo, amesema madereva, wamiliki na watumishi wa Serikali wasio waaminifu ni sehemu ya tatizo.

Khatibu Hamidu, mtaalamu wa masuala ya vipimo amesema mizani inaweza kutofautiana majibu kama mmoja umepata hitilafu ya kuyumba baada ya lori kuingia kupimwa.

“Mzani unaweza kuyumba, lori la mizigo linaweza kupimwa eneo la kwanza na la pili ukaonekana sawa na eneo la tatu mzigo ukaonekana hauko sawa kutokana na hitilafu ya mzani ambayo inaweza kusababishwa na lori lenywe.

“Mizani yote inapaswa kuwa sawa kama majibu hutofautiana kidogo sana lakini vipo viwango vilivyopendekezwa kwamba mzigo ukizidi hauna shida, lakini ikionekana majibu tofauti zaidi na yaliyoonekana kupitia mizani mingine kuna shida ya mzani husika,” amesema.

Amesema kwenye suala la upimaji vipimo havipaswi kutofautiana na kama kutatokea changamoto, Wakala wa Vipimo (WMA) anapaswa kwenda kuhakiki ubora wa mzani husika.

Kahamba Anthony, mtaalamu wa mizani amesema yapo mambo matatu yanayoweza kuchangia uzito wa mzigo kuonekana tofauti kati ya mzani mmoja na mwingine hususani kwa magari ya mizigo.

Jambo la kwanza ni hitilafu ya mizani yenyewe, dereva kuongeza mafuta kwenye gari baada ya kutoka kwenye mzani wa kwanza au kuongezwa mzigo.

“Kama mzigo umezidi kwa kiwango kikubwa mafuta hayawezi kuchangia ongezeko hilo, huenda dereva aliongeza mzigo njiani na kama sivyo, basi mzani utakuwa umepata hitilafu ndiyo maana majibu yakaja tofauti mizani nyingine,” amesema.

Related Posts