Dar es Salaam. Suala la upatu na mikopo umiza limeendelea kuumiza vichwa vya Watanzania, safari hii Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir akisimuliwa ambavyo amewahi kuokoa watu walotaka kuangamizana kisa michezo hiyo.
Mufti Zubeir ameeleza hayo wakati wa futari iliyoandaliwa na Benki kuu ya Tanzania (BoT) jana, akisisitiza kuwa suala la elimu na uadilifu katika huduma za kifedha si la kuwaachia wananchi, badala yake kila mtu anapaswa kushiriki.
Sheikh Zubeir ambaye hakuelezea kwa kina visa alivyowahi kukutana navyo, alisema kutokana na umuhimu wa huduma za kifedha kwa watu, BoT inapaswa kuendelea kutoa elimu ili wananchi waweze kufanya shughuli zao kwa uzuri.
“Unakuta watu wameanzisha upatu baadaye wanataka kuchinjana, mimi mwenyewe nilishaokoa baadhi ya watu ambao walianzisha upatu baadaye wakataka kuangamizana, hivyo Benki Kuu endeleeni kutoa elimu kama njia mojawapo ya kulinda amani,” amesema.
Amesema suala la elimu ya fedha wasiachiwe wananchi pekee kwani ni muhimu watu wakajua namna bora ya kutumia fedha, kuchukua mikopo, namna ya kurejesha na hata ufunguaji na usimamizi wa biashara.
Amesema Uislamu umezungumza masuala ya utunzaji wa fedha, kuishi kiuchumi na namna ya kutumia.
Akifafanua, alisema kuna sura inaeleza kuwa anayetumia wastani katika maisha Mwenyezi Mungu anamfanya aweze kuishi vizuri na kuwa na akiba kwa ajili ya maisha yake na anayetumia hovyo anasozwa mpaka anakuwa fukara.
Katika hafla hiyo iliyohudhuria na wakuu wa taasisi za fedha nchini pamoja na makundi mengine, Mwalimu Salum Othuman alitoa darasa la usimamizi wa fedha katika muktadha wa dini na alishauri watu kufuata maelekezo na ushauri wa wataalamu katika kufanya miamala ya fedha, ili kuwa na sekta ya fedha imara iliyojengwa katika uadilifu na kweli kwa manufaa ya uchumi wa nchi.
“Wasomi wote wa masuala ya kifedha wanakubaliana kuwa masuala yasiyo ya kiungwana yanaposhamiri yanasababisha kukosekana kwa uthabiti wa sekta na kuathiri uchumi. Uadilifu katika miamala ya fedha unaweza kuchangia uthabiti wa sekta ya fedha,” alisema.
Awali katika futari hiyo, Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba naye alilia na upatu akisema katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la huduma za fedha nchini, lakini mafanikio hayo yamekumbwa na changamoto hususani kwenye huduma ndogo za kifedha.
“Kuna mikopo umiza wengine wanaiita kausha damu, lakini pia kuna wale wanaotoa mikopo yenye riba kubwa, wengine wanatoa huduma za kifedha bila leseni, wengine mtandaoni huku wengine wakifanya utapeli kwenye shughuli za upatu,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, Gavana alitoa wito kwa wananchi kujiepusha na shughuli za upatu na kuhakikisha wanapata huduma za kifedha kwa watoa huduma wenye leseni halali ya Benki Kuu au taasisi zilizokasimishwa mamlaka.
“Natoa rai kwa watoa huduma nchini wenye leseni kuhakikisha kuwa wanatoa huduma zinazokidhi mahitaji na zisizowaumiza Watanzania wenzetu na kuhakikisha wanafuata masharti yote ya leseni, la si hivyo Benki Kuu itafuta leseni hizo na kuwachukulia hatua za kisheria,” amesema Tutuba.
Mufti Zubeir na Tutuba wameeleza hayo kipindi ambacho masuala ya upatu wayekuwa tatizo kubwa nchini, na hivi karibuni Raia mmoja China, Weng Jianjin alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka matatu, yakiwamo ya kukusanya na kuendesha biashara ya upatu na kujipatia Sh34.7 bilioni kwa njia ya udanganyifu.
Mbali na suala la Upatu, Mufti alisema mwezi Ramadhani ni chuo cha kujifunza kuhusu dini na maadili na katika kipindi hicho watu wanapendana, wanajengana, wanakuwa na subira, kustahimiliana na kufundishana.
“Katika mwezi wa Ramadhani tunajifunza kutunza amani ya mtu na mtu, familia na familia, na watu wote kwa tofauti zao, unatufunza namna ya kuaminiana baina ya Waisilamu na wasiokuwa Waisilamu, dini inafundisha hata namna ya kuishi na watu wasiokuwa Waislamu,” alisema.
Alisema dini inaelekeza kuwa Waisilamu waaminiane na wasiokuwa Waislamu, wakae nao kwa wema, washirikiane nao katika mambo mazuri ambayo yanaleta amani, utulivu, mshikamano na umoja katika dunia.
Aidha Mufuti alisema mwaka huu ni muhimu sana katika kufikiria suala la amani, kuzuia na kuziba viashiria ambavyo vinaweza kusababisha kuharibika kwa amani katika nchi akisema kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ni kimbilio la amani kwa mataifa mengi.
“Ni mwaka ambao tunahitaji kujitambua, ni mwaka ambao kama mtu ana fikra zake za hovyo hovyo abadilike aone umuhimu wa kutunza amani katika nchi yetu, nchi nyingi zilizotuzunguka zinaitazama Tanzania kama nchi yenye amani,” alisema Mufti.
Naye Tutuba alisema kipindi hiki (cha Ramadhan) kinatoa chachu ya kudumisha amani na utulivu kwa mtu mmoja mmoja, familia, taifa na kimataifa na kuwa kila mtu ana wajibu wa kulinda amani iliyopo kwa kuzingatia maelekezo ya viongozi na kufanya kazi ili kupata kipato halali.
“Kwakuwa huu ni mwaka wa uchaguzi, napenda kutumia nafasi hii kutoa rai kwa wote kuendelee kuliombea taifa ili uchaguzi utakapofanyika tupate viongozi wenye hofu ya Mungu. Uchaguzi ufanyike vizuri kwa uhuru na haki na amani ya nchi yetu iendelee kutawala,” alisema Tutuba.