Mwanza. Mwili wa mwanamke aliyekutwa amefariki dunia katika nyumba ya kulala wageni ya First and Last, ukiwa umefungwa kitambaa usoni, eneo la Usagara Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, umetambuliwa.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Ijumaa Machi 21, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema marehemu alikuwa mkazi wa Buchosa, Wilaya ya Sengerema mkoani humo.
Amesema mwili wa mama huyo ametambuliwa na watoto wake pamoja na ndugu wengine na kwamba uchunguzi utakapokamilika utakabidhiwa kwao kwa ajili ya mazishi.
“Watoto wake na ndugu wengine wamejitokeza na kumtambua, hivyo watakabidhiwa mwili wa ndugu yao baada ya post mortem (uchunguzi) ili wakampumzishe ndugu yao,” amesema Mutafungwa.
Mutafungwa amesema mtuhumiwa wa tukio hilo bado hajakamatwa.
Mama huyo anadaiwa kuuawa usiku wa kuamkia Machi 19, 2025 baada ya kuingia katika chumba cha gesti hiyo na mwanaume aliyejiandikisha kwa jina la Bilal William, mkazi wa Geita aliyefikia kwenye nyumba hiyo akitokea Chato akielekea Nzega mkoani Tabora.
Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa, William alipewa chumba namba tatu na kuweka mizigo yake, ilipofika saa 4 usiku, alitoka akidai anakwenda kutafuta chakula na ilipofika usiku mnene alirudi katika chumba chake na kulala akiwa na mwanamke huyo.
“Inadaiwa ilipofika saa 12:00 asubuhi wakati wahudumu wa nyumba hiyo wakihitaji kufanya usafi, ndipo walipokuta mlango wa chumba ukiwa na komeo lililofungwa kwa nje, hali hiyo iliwatia mashaka, hivyo wakafungua kufuli hilo na kuingia ndani.
“Ndipo walipoona kuna mwanamke amefungwa usoni kwa kitambaa akiwa na mikwaruzo usoni mwake huku akiwa mtupu. Mwanaume aliyepangisha chumba hicho hakuwepo,” amesema Mutafungwa.