Nchi za ukanda wa Afrika Mashariki kutumia nembo moja soko la hisa

Dar es Salaam. Umoja wa masoko ya Hisa katika nchi za Afrika Mashariki unatarajia  kutambulisha nembo moja ya soko la hisa katika ukanda huo, lengo likiwa kuwavutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya ukanda huo.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Machi 21, 2025 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), Peter Nalitolela alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo mbalimbali waliyojadiliana katika mkutano mkuu wa mwaka wa umoja huo, uliofanyika kwa siku tatu jijini Dar es Salam.

Nalitolea amesema malengo ya kuja na nembo hiyo ni kutambulisha umoja huo, lakini kubwa kuwavutia wawekezaji katika maeneo mbalimbali.

Kuhusu mkutano huo, amesema ulilenga   kuangalia fursa zilizopo katika masoko yao kwa pamoja ukibeba kaulimbiu ya ‘Soko moja, fursa zisizo na ukomo’

“Wote tunaangalia uwekezaji wa pamoja  kuangalia namna wananchi wetu wanaweza kuwekeza na namna ya kupata mitaji ili kufaidika na soko la hisa na ndio maana tumeona pia kuna haja ya kuwa na nembo moja ya kutambulisha soko letu la Afrika Mashariki,” amesema.

Vilevile kwa ushirikiano huo, amesema wanapata nguvu moja ya uwekezaji ukizingatia kuna masoko yalikuwepo kwa muda mrefu kama la Nairobi lakini pia kuna masoko mengine mapya yamekuja ikiwemo ya Ethiopia na Somalia, hivyo wanakuwa na uwezo ya kuyazungumzia yote kwa pamoja ili kuwavutia wawekezaji.

Akizungumzia kuhusu changamoto zilizopo katika uwekezaji huo wa masoko ya hisa katika nchi hizo, amesema bado wananchi hawajawa na uelewa kuhusu masoko ya mitaji na dhamana.

Changamoto nyingine amesema ni miundombinu ya ndani ambayo kama mwekezaji wa Kenya anataka kuwekeza Kenya au Uganda, atawezaje kuunganishwa katika mfumo mmoja.

Kwa upande wa kampuni amesema bado kuna ambazo  zipo tayari kwenda kukopa kwingine lakini si kwenda kuwekeza katika masoko hayo ya mitaji , hivyo kwa umoja huo pamoja na mambo mengine watakuwa wakishirikiana katika utoaji elimu wa umuhimu wa kuwekeza katika masoko ya hisa.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa masoko ya Hisa Afrika, Pierre Rwabukumba amesema  hatua hiyo ni mwanzo mzuri wa kulifikia soko la Afrika na yale ya kimataifa.

“Unapokuwa na umoja  wa Kikanda, utasaidia kukuza biashara kwa nchi za Afrika na hatimaye kuyafikia kirahisi masoko ya kimataifa,” amesema Rwabukumba ambaye pia ni ofisa mtendaji mkuu wa soko la hisa nchini Rwanda.

Ameongeza kuwa Afrika ina kila sababu kufanya biashara yake yenyewe  na ikawezekana kutokana na mtaji wa idadi kubwa ya watu lililonao  ambao wengi wao ni vijana.

 “Hivyo tunachokifanya hapa ni kuleta nguvu pamoja kulifikia soko la hisa duniani ambapo kwa nchi za wenzetu zilizoendelea kwao ni injini ya uchumi, hivyo tutaweza kuwavutia pia wawekezaji kutoka nje ya bara letu kuja kuwekeza kwetu,” amesema mwenyekiti huyo.

Naye Mwenyekiti wa Masoko ya Hisa Afrika Mashariki, Paul Bwiso amesema katika siku hizo tatu wamejadiliana mambo mbalimbali yakiwemo ya kiufundi na namna gani ya kuja na mikakati ya pamoja kwa ajili ya wananchi kushiriki vilivyo katika biashara za soko la hisa.

Bwiso amesema nchi zilizo katika umoja huo ukiacha Tanzania, ipo Ruanda, Burundi, Uganda , Ethiopia Somalia na Kenya

Related Posts