Dar es Salaam. Wakati ripoti mpya ikionyesha asilimia 63.4 ya taka zinazozalishwa jijini Dar es Salaam ni zinazooza, wadau wameshauri kampeni za kukabiliana nazo ikiwa moja ya njia za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Taka hizo ambazo kwa kiasi kikubwa zinatokana na mabaki ya chakula na matunda, zinapooza hutoa gesijoto kama methane na kaboni, hivyo kuchochea mabadiliko ya tabianchi na mafuriko pale zinapoziba mifereji wakati wa mvua.
Ripoti ya Dar es Salaam Urban Resilience Project (DURP) ya Machi 13, 2024 inaeleza, “taka hizo husababisha mabadiliko ya tabianchi, zisizodhibitiwa huachwa kando mwa barabara, mito au mifereji, zikiharibu mazingira.”
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 57 ya taka jijini Dar es Salaam huishia mitaani kati ya tani 5,300 zinazozalishwa kila siku, huku tani 1,500 pekee zikifikishwa dampo. Kati ya taka hizo, zaidi ya asilimia 60 ni zinazooza.
Ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) inaonyesha tani bilioni 1.3 za chakula hupotea kila mwaka, na kuzalisha tani bilioni 3.3 za gesijoto, sawa na asilimia nane hadi 10 ya uzalishaji wa gesijoto duniani.
Wadau wanapendekeza mikakati madhubuti ya urejelezaji na utengenezaji wa mbolea kutokana na taka zinazooza ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 kifungu cha 114 inazipa wajibu wa kutekeleza mamlaka ya serikali za mitaa kusimamia na kupunguza taka. Kwa kiwango kikubwa huzalishwa majumbani na sokoni.

Wakusanya taka wa sekta isiyo rasmi (waliovaa fulana za njano) Kurasini, Temeke, wakionyesha taka zilizotengwa tayari kwa kukabidhiwa kwa mkusanyaji mkuu eneo hilo.
Kiongozi wa tafiti na mshauri wa masuala ya maendeleo, Mansoor Ali anasema wamefanya tafiti sita kwenye mradi wa DURP mwaka 2024 kwa ufadhili wa Serikali ya Uingereza.
Anasema miongoni mwa maeneo waliyoyabaini ni kuwajengea uwezo wasimamizi wa taka wa manispaa ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Wasimamizi wa taka waachane na mnyororo uliozoeleka wa usimamizi wa taka unaoanza na uzalishaji kisha mkusanyaji anayepeleka dampo, badala yake taka zitenganishwe kwenye chanzo na zifanyiwe kazi kulingana na aina yake. Hili linaongeza thamani ya taka na kupunguza athari za mazingira,” anasema.
Mansoor anasema maofisa hujengewa uwezo mara chache, pasipokuwa na mwendelezo, hivyo kuwapo tatizo katika utekelezaji.
“Tumewajengea uwezo maofisa zaidi ya 20, ambao tunatarajia wakaboreshe kampeni za mazingira zilizopo na watakazobuni zijumuishe masuala ya mabadiliko ya tabianchi ili kuendana na hali halisi ya dunia kwa sasa,” anasema.
Akizungumzia elimu waliyopewa, kiongozi na mwakilishi mkuu wa maofisa hao, Geophrey Zenda anasema: “Taka hasa za kuoza zinazalisha hewajoto ambazo ni hatari kwa mazingira. Katika elimu tunazotoa ni utenganishaji taka, udhibiti mzuri na kuchakata zile zinazowezekana.”

Wananchi wa Vingunguti na wadau wakifanya usafi wa katika daraja la Kwa Kombo. Usafi huu ulilenga kusafisha mifereji, madaraja ili kupunguza athari za mafuriko na mazingira.
Zenda, ambaye pia ni ofisa afya mazingira mkuu katika Wilaya ya Ilala, anasema walijifunza zaidi udhibiti wa taka unavyofanyika maeneo mengine duniani kabla ya kuja kuwaelekeza wenzao nchini.
Anasema Pune, nchini India wakusanya taka wa sekta isiyo rasmi walisajiliwa tangu 2008, wakisaidia kukusanya na kuzitenganisha kabla ya manispaa kuzikusanya. Pia, matumizi ya nishati itokanayo na taka (biogas) yanahamasishwa katika kaya na migahawa kama nishati mbadala.
Zenda amesema mafanikio yanategemea ushirikishwaji wa jamii, takwimu sahihi, miradi bunifu, ushirikiano wa sekta binafsi, uwezeshaji wa wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi, sera bora, tathmini ya miradi na mabadiliko ya tabia.
Naada ya kupatiwa mafunzo, Ofisa Afya na Mazingira wa Halmashauri ya Kigamboni, Sixbert Kyaruzi anasema Machi 12, 2024 walifanya kampeni ikiwa na kaulimbiu “Kigamboni: Usafi ni mimi na wewe” ikilenga kuelimisha jamii kwa kusisitiza usafi wa mazingira na kutenganisha taka.
Shakukle Jafari, mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ungindoni ambako usafi ulifanyika sokoni, alisema eneo hilo huzalisha taka kwa wingi.
Elimu hiyo pia imewafikia wananchi wa Kurasini, Wilaya ya Temeke, kuhusu fursa zilizopo kwenye taka kupitia kampeni ya mazingira iliyofanyika Machi 14 na 15, 2025.
Elimu hiyo ilitolewa na wadau wa mazingira wakiongozwa na Ofisa Afya wa Kata ya Kurasini, Imani Rajabu, kwa kushirikiana na kampuni za wadau wengine wa mazingira.
Kwa mujibu wa Rajabu, taka si uchafu bali ni mali inayoweza kuleta kipato, akisema wamefundisha wananchi jinsi ya kuzitumia kuboresha maisha na mazingira yao.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mivinjeni, Mwamtum Gumbo anasema: “Elimu hii itakwenda kupunguza taka mtaani kwani awali wananchi waliona kama haiwezekani taka kuwa mali, kizuri zaidi hapa mtaani kuna mtu ameanzisha kiwanda kidogo cha kununua taka hiyo kuleta hamasa zaidi.”
Mmiliki wa kiwanda hicho, Dotto Maliatabu, anasema licha ya mchango wake katika kuchakata taka, anakumbana na changamoto kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Serikali wanaodai anachafua mazingira.
Hata hivyo, anasema amekuwa akiwaelimisha kuhusu umuhimu wa shughuli yake katika usafi wa mazingira.
Kwa upande wao, wakazi wa Mtaa wa Kwa Kombo, uliopo Vingunguti wamesafisha madaraja mtaani na kwenye soko la Kwa Simba ikiwa ni hatua ya kujiandaa kwa ajili ya msimu wa mvua.
Katika kampeni hiyo iliyoongozwa na ofisa afya wa Kata ya Vingunguti, Amisa Mtendawema Machi 15, 2025, vikundi vya kijamii vilishiriki.
Kwa upande wake mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kwa Kombo, Athumani Musa, amesema usafi uliofanyika kwenye soko la Kwa Simba ni muhimu kwani hakuna mkandarasi maalumu wa kukusanya taka.
Kikundi cha Ilala Jogging, kikiongozwa na Hassani Samakimkubwa, kilishiriki usafi Vingunguti.
Amesema kampeni ya usafi kila wiki imepunguza magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu, hasa katika msimu wa mvua.
Halmashauri ya Kinondoni kupitia kaulimbiu ya “Mguu kwa mguu kitaa” ilifanya usafi Mtaa wa Kwa Kopa Mwananyamala Machi 18, kwa kutembelea nyumba kwa nyumba kudhibiti taka kuanzia majumbani.
Ofisia Mazingira na Afya wa Kinondoni, Alban Mugyabuso alitaja malengo ya mradi huo ni kuongeza uelewa, kusafisha mazingira, kukabili magonjwa ya milipuko na kuongeza uchumi wa wananchi kwa kuongeza thamani ya taka.
Halmashauri ya Ubungo ikiongozwa na ofisa usimamizi wa mazingira, Anna Kitutu alisema: “Tunapanga kutumia kituo cha Mabasi cha Magufuli kwa kutumia kipaza sauti kuhamaisha uhifadhi wa mazingira na kufanya usafi pamoja na wananchi,” alisema.