RUWASA MANYARA KUTUMIA BAJETI YA BILIONI 19 KWA MWAKA 2025/2026

Na Mwandishi wetu, Babati

MAMLAKA ya maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Mkoa wa Manyara imelenga kutumia shilingi 19,976,897,468.78 ya kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026.

Mkoa wa Manyara una jumla ya vijiji 440 kati ya hivyo, vijiji 396 vinahudumiwa na RUWASA ambapo vijiji 329 vina huduma ya maji na vijiji 67 havina huduma ya maji ya uhakika.

Hayo yameelezwa na Meneja wa RUWASA Mkoa wa Manyara, James Kionaumela, akizungumza kwenye kikao cha ushauri kamati ya mkoa huo (RCC) kilichofanyika hivi karibuni mjini Babati.

Kionaumela amesema mpango huo wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2025/2026 umezingatia maagizo ya viongozi mbalimbali wa ngazi ya kitaifa yaliyotolewa maeneo husika akiwemo Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu, Waziri wa Maji na Naibu Waziri wa Maji.

“Kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati na kukamilisha miradi inayoendelea, kufanya upimaji wa uwepo wa maji chini ya ardhi, kuchimba na kujenga eneo la kuchotea maji karibu na kisima,” amesema.

Meneja huyo amesema pia mpango huo umelenga kupeleka huduma ya maji katika vituo vya afya, zahanati, shule za msingi na sekondari ambazo hazina huduma ya maji.

Amesema jumla ya miradi 26 ya thamani ya shilingi 16,339,414,270.41 imekamilika na miradi 18 yenye thamani ya shilingi 59,532,140,530.20 inaendelea na utekelezaji.

Hata hivyo, amesema hadi Desemba 31 mwaka 2024, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwenye vijiji mbalimbali vya mkoa huo ni asilimia 71.

Amesema kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Babati ni asilimia 80.9, Wilaya ya Kiteto asilimia 64, Wilaya ya Simanjiro asilimia 66.7 Wilaya ya Hanang’ asilimia 71.2 na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu asilimia 69.7.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Cuthbert Sendiga amepongeza utendaji kazi wa RUWASA katika kutoa huduma mbalimbali za jamii kwenye eneo hilo.

Related Posts