WACHEZAJI wa Yanga wamerejea mazoezini baada ya kuwa na mapumziko ya takribani wiki moja tangu watoke kuichapa Coastal Union mabao 3-1 katika mchezo wa hatua ya 32 bora michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), Machi 12 mwaka huu.
Kabla ya kucheza na Coastal, Machi 8 mwaka huu Yanga ilitarajiwa kuikabili Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, lakini uliahiarishwa na Bodi ya Ligi Kuu Bara.
Kukaa wiki moja bila ya kucheza mechi, ndiyo sababu imemfanya Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi kuwarejesha mazoezini mastaa wake ikiwa ni siku nne kabla ya kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Singida Black Stars.
Jumatatu ya Machi 24 mwaka huu, Yanga na Singida Black Stars zinatarajiwa kucheza mechi hiyo ya kirafiki kwa ajili ya kuzindua uwanja utakaokuwa unamilikiwa na Singida.
Nyota wote ambao hawana majukumu kwenye vikosi vyao vya timu za taifa wameitwa na Hamdi kwa ajili ya kujiweka tayari na safari ya kwenda Singida Jumamosi Machi 22 kwa ajili ya mchezo huo utakaopigwa Jumatatu ijayo.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo mwenye mbinu kali uwanjani, alisema wanahitaji kujiweka sawa mapema kabla ya mchezo huo kwani hawajacheza muda mrefu.
Hata hivyo, Hamdi amebainisha kuwa wanakwenda kucheza mchezo muhimu kwao kutokana na timu hiyo kutokuwa na mechi kwa muda mrefu huku akisisitiza ni wakati sahihi wa wachezaji wake kuonyesha uwezo hasa wale ambao wamekuwa wakikosa nafasi ya kucheza.
“Natarajia mchezo mzuri na bora kutoka kwa Singida Black Stars kutokana na kuwa na nyota wengi bora na wazoefu, naifahamu vizuri timu hiyo pamoja na kwamba sipo hapa nchini muda mrefu.
“Ni kipimo kizuri kwetu na ni muda sahihi kupimana nao nguvu na kubaini ubora wao na mapungufu yao yakiwa ni maandalizi sahihi ya michezo yetu ijayo ya ligi,” alisema kocha huyo.
Miloud alisema hana kawaida ya kuhofia mchezaji wa timu pinzani, anatishika na mbinu za makocha uchezaji ni namna ambayo mchezaji mmoja mmoja anaonyesha ubora wake.
“Sina kawaida ya kumuhofia mchezaji yeyote, natambua ubora wao lakini mbinu sahihi ndio zinaamua matokeo pale wachezaji 22 wanapokutana, nakiamini kikosi changu na nawaheshimu wapinzani.”
Yanga kwenye kikosi chao wanatarajia kuwakosa Djigui Diarra, Dickson Job, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Khalid Aucho, Duke Abuya, Clatous Chama, Kennedy Musonda, Mudathir Yahya, Prince Dube na Clement Mzize ambao wameitwa na timu zao za taifa.
Hivyo nyota wengine wote wa kikosi hicho waliosalia akiwemo Aziz Ki na Pacome Zouzoua watakuwa sehemu ya wale watakaenda kucheza mchezo huo.
Singida BS itakuwa timu ya nne kwenye Ligi Kuu Bara kumiliki uwanja baada ya Azam, JKT Tanzania pamoja na KMC Complex.