Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema umoja na mshikamano ndiyo silaha pekee itakayoiwezesha Afrika kuzikabili changamoto zinazoendelea katika mataifa yake, ikiwemo vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Amesema Afrika ya sasa imebaki kuwa na mataifa ambayo mipaka yake si salama tena na hata dhana ya ujirani mwema imezidiwa na migogoro ya ndani.
Kauli hiyo ameitoa wakati ambao baadhi ya mataifa ya Afrika yanakabiliwa na machafuko, kama Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Sudan.
Rais Samia amesema hayo nchini Namibia leo, Ijumaa Machi 21, 2025 alipohutubia kwenye sherehe za uapisho wa Rais mpya wa Taifa hilo, Netumbo Ndaitwah.
Katika sherehe hizo ambazo Rais Samia alikuwa mgeni rasmi, amesema mipaka ya mataifa ya Afrika kwa sasa si salama tena na hata dhana ya ujirani mwema imegubikwa na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe kuliko vita vya mipaka vilivyoshuhudiwa zamani.

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi mbalimbali baada ya hafla ya uapisho wa Rais mteule wa Jamhuri ya Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah iliyofanyika katika Ikulu ya nchi hiyo Windhoek leo Ijumaa Machi 21, 2025.
“Katika kukabiliana na changamoto hizi, nguvu zetu zimebaki kwenye umoja na mshikamano wa Afrika. Lazima tutafsiri maana ya mshikamano wetu kwa ajili ya leo na baadaye,” amesema.
Amesema mataifa ya Afrika yanapaswa kusimama kama msaada kwa yenyewe kwa yenyewe, badala ya kuwa kikwazo.
Katika kipindi ambacho siasa za dunia zimetawala, amesema ni muhimu kwa mataifa ya Afrika kushirikiana yakijua ushindi utatokana na utawala bora na wa sheria.
Amesema changamoto zilizowakabili waasisi wa mataifa hayo zamani, si zilizopo sasa kwa kuwa kipindi hiki dunia inahitaji kuwaondoa wananchi kutoka kwenye umaskini, njaa na changamoto za ulinzi.
“Uchumi wetu umepitwa na kugubikwa na mizania isiyo sawa ya kibiashara wakati idadi ya watu inaongezeka, huku ikolojia ikiendelea kuharibika,” amesema.
Mbali na changamoto hizo, amesema Namibia si tu inasherehekea siku yake ya kitaifa, bali inaandika historia ya kumuapisha Rais wa pili mwenye jinsi ya kike katika Bara la Afrika.
“Mnaposherehekea miaka 35 ya uhuru wa Taifa lenu niwatakie furaha ya uhuru na mfurahie sherehe hizo mbili za kuandika historia yenu,” amesema.

Amesema ushindi wake katika kiti hicho umejenga hamasa kwa mabinti ndani ya Namibia.
“Kwetu Tanzania tunafurahia kuona mtoto tuliyemfunza na kumlea kwa upendo sasa amekua na kuwa katika ofisi kuu ya Taifa. Mheshimiwa Rais majirani zako pale Magomeni, wanakusherehekea na wamekutumia salamu za pongezi,” amesema Rais Samia.
Amesema Rais Ndaitwah amefanya kazi kubwa kusaidia kile kilichohitajika kwa ajili ya chama chake cha Swapo katika miaka ya 1980 hadi 1986 akiwa Tanzania.
“Nasema haya leo kwa sababu nataka dunia itambue kwamba, Watanzania na Wanamibia ni ndugu waliotenganishwa tu na mipaka ya kijiografia,” amesema.
Samia amesema nchi hizo mbili zimekuwa kinara katika kuwezesha masuala ya uwezeshaji wanawake na usawa wa kijinsia.
“Kama mtakumbuka wanawake shupavu wa Tanzania na Namibia ndio waliochora mstari wa majadiliano kuhusu masuala hayo. Kwa upande wa Tanzania ni Gertrude Mongella, alihudumu kama Katibu Mkuu wa Mkutano wa Beijing mwaka 1995, akisaidiana na Netumbo Ndaitwah,” amesema.
Amesema si bahati mbaya kwa mataifa hayo baada ya miaka 30 ya Beijing kwa sasa yana viongozi wakuu wa nchi wanawake.
Akihutubia hafla hiyo iliyohudhuriwa na wakuu wa nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo DRC, Felix Tsishekedi, Rais Ndaitwah amesema jukumu lake ni kuendeleza yaliyofanywa baada ya uhuru na kukamilisha ajenda zilizosalia.
“Majukumu yangu yapo wazi kupitia ilani ya uchaguzi ya Chama cha Swapo na huo ndiyo utakaokuwa mwongozo wangu, nitasimama na Wanamibia wote bila kujali itikadi zao za kisiasa,” amesema.
Amesema Serikali chini ya Swapo imekuwa ikitekeleza ajenda ya usawa katika uongozi ndani ya Serikali na yeye ni miongoni mwa waliotokana na hilo.
Ingawa wamepiga hatua kuhusu usawa wa kijinsia katika Taifa hilo, amesema bado kuna mengi yanayopaswa kufanywa katika kufikia usawa wa asilimia 50 kwa 50.
“Naomba ieleweke kwamba, sikuchaguliwa kwa sababu ni mwanamke, bali kwa vigezo. Hivyo nisema wanawake hatupaswi kuomba kuchaguliwa katika nafasi za uwajibikaji eti kwa sasa tu wanawake, bali kwa sababu ni watu wenye uwezo ndani ya jamii wa kushika nyadhifa hizo,” amesema.