Dar es Salaam. Neema ya uhakika wa upatikanaji wa chanjo yenye ubora kwa wafugaji inanukia, hii ni baada ya Serikali kupokea majokofu zaidi ya 60 yaliyotolewa na kampuni zinazozalishaji chanjo hizo.
Majokofu hayo yatawezesha chanjo za mifugo kuhifadhiwa katika hali nzuri pindi Serikali itakapoanza rasmi mchakato wa usambazaji wa dawa hizo za kinga katika halmashauri zote 184.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa, Machi 21, 2025 muda mfupi baada ya kupokea majokofu 60 kati ya 100 yaliyotolewa na kampuni ya kuzalisha chanjo ya Hester Bioscience Africa Ltd (HBAL), Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji amewataka wafugaji kukaa mkao wa kula kuhusu upatikanaji wa chanjo.
“Wafugaji wamekuwa na maswali kwamba tulianza kampeni ya usambazaji wa chanjo, sasa mbona tunachelewa? Niwaambie hatujachelewa, bali yalikuwa maandalizi ambayo mojawapo ni upatikanaji wa majokofu.
“Sasa tunakwenda kuyasambaza halmashauri za mikoa yote Tanzania Bara, wafugaji wasiwe na wasiwasi bali wawe tayari kwa sababu muda umefika wa kuanza chanjo kwa ajili ya mifugo yetu,” amesema Dk Kijaji.
Akizungumzia kuhusu Hester Bioscience Africa Ltd (HBAL), Dk Kijaji amesema ni mojawapo ya kampuni tatu zilizoingia mkataba wa makubaliano na Serikali kwa ajili ya kusambaza chanjo, huku zikitakiwa kutoa majokofu 184 kwa ajili ya kuhifadhia kinga hiyo ili isiharibike.
“Zipo chanjo zinazotakiwa zihifadhiwe chini ya nyuzi joto 20 na nyingine 16°C na kuendelea. Majokofu 60 yaliyotolewa hapa ni sehemu ya majokofu 184 yatakayosambazwa kwenye halmashauri zote nchini.
“Tulikubaliana na Hester Bioscience Africa Ltd, watoe majokofu 100, wameleta 60 yaliyobaki wataendelea kuyatoa, wakati kampuni mbili zilizobaki zilitakiwa kutoa majokofu 84. Kati ya 84, majokofu 40 yameshatolewa yapo jijini Mwanza,” amesema.
Dk Kijaji ametumia nafasi hiyo kuipongeza kampuni ya Hester Bioscience Afrika Ltd, kwa kutoa majokofu hayo na maandalizi yakikamilika uzinduzi rasmi utafanyika.
Kampuni nyingine zilizoingia makubaliano hayo na Serikali ni Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) na Novel Vaccine and Biological Limited (Novabi).
Ofisa Mtendaji Mkuu na Mkurugenzi Mtendaji wa Hester Bioscience Afrika Ltd, Rajiv Gandhi amesema wanafurahi kuwa sehemu ya taasisi inayounga mkono kampeni ya kitaifa ya upatikanaji wa chanjo.
“Leo ni siku kubwa kwetu katika kuhakikisha usambazaji wa chanjo unafika katika maeneo yote, tunasikia faraja kwa ushirikiano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi (Dk Kijaji), tumechangia majokofu 60 kwa ajili ya kuhidhafia chanjo yatakayopelekwa katika maeneo maalumu nchini.
“Huu ni mwanzo wa mpango wa kitaifa wa usambazaji wa chanjo, na katika kampuni tunazalisha chanjo mbili za PPR na CBPP kwa ajili ya mifugo, tumejizatiti katika kukinga mifugo kuondoka na magonjwa kupitia chanjo zetu,” amesema Gandhi.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetenga Sh28.1 bilioni katika mpango wa utoaji wa chanjo na utambuzi wa mifugo, hatua itakayowezesha kudhibiti na kutokomeza magonjwa ya mifugo nchini.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, awamu ya kwanza ya mpango wa chanjo, Serikali kupitia wataalamu wa sekta ya mifugo na Mamlaka za Serikali za Mitaa, itachanja ng’ombe 19,097,223 dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu ya ngo’mbe (CBPP).
Pia, itachanja mbuzi na kondoo 20,900,000 dhidi ya ugonjwa wa Sotoka (PPR) na kuku wa asili 40,000,000 dhidi ya ugonjwa wa mdondo wa kuku (ND), lengo la Serikali ni kutoa chanjo kwa mifugo angalau asilimia 70 ya idadi ya mifugo husika kwa miaka mitano mfululizo.