Serikali kuwaanika hadharani ‘tuma kwa namba hii’

Songwe. Naibu Waziri Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi amesema wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani watawaweka hadharani waharifu wa mtandaoni wanaotuma ujumbe wa maneno wa “tuma kwa namba hii”.

Mahundi ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Machi 21, 2025 katika Kituo cha Pamoja cha Forodha kwenye mpaka wa Tunduma mkoani Songwe ikiwa ni siku ya pili ya ziara yake ya kukagua mwingiliano wa mawasiliano baina ya Tanzania na nchi jirani ya Zambia.

Kauli hiyo imefuatia malalamiko ya Mkuu wa Wilaya ya Momba, Elius Mwandobi kumueleza kuwepo kwa wimbi la matapeli mtandaoni ambao wamekuwa kero kwa jamii.

Pia, amewanyooshea kidole mawakala wanaosajili laini za simu kuhusika kutapeli wakulima kwa kutumia mbinu za kusajili laini na kisha kuhamisha fedha, jambo ambalo limelalamikiwa.

“Naibu Waziri, tunaomba kujua mikakati ya serikali kukabiliana na wimbi hili kwani imekuwa kero kubwa, mimi binafsi hizo meseji za “tuma kwa namba hii” nazipata zinanipa kero kubwa,” amesema.

Amesema ili kukomesha uharifu unaofanywa mitandaoni, ni wakati sasa serikali kuweka mikakati ya kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua ili kudhibiti matukio hayo kutojirudia.

“Changamoto nyingine ni baadhi ya kampuni kutoshirikisha viongozi wa serikali wanapoingia kwa wananchi kutoa huduma, ndio mwanya ambao hutumiwa na mawakala wanaosajili laini kuwaibia wakulima, kumekuwa malalamiko mengi,” amesema.

Mwandobi ameyataka kampuni ya simu kushirikisha watendaji wa serikali sambamba na kutoa vitambulisho vya mawakala wanaosajili laini ili kuwabaini wasio wahaminifu,” amesema.

Katika hatua nyingine ameomba mamlaka husika kuboresha upatikanaji wa mawasiliano katika baadhi ya maeneo ukanda wa ziwa Rukwa ili wananchi kufikiwa na huduma hiyo muhimu ya matumizi ya mifumo ya kidigitali.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Mhandisi Maryprisca Mahundi ameonya kampuni ya simu kuacha tabia ya kutoa ajira kiundugu ya usajili wa laini ili kukabiliana na matukio ya uharifu.

Katika hatua nyingine, amesema Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi watalisaidia Jeshi la Polisi kuwaweka wazi waharifu wa mtandaoni kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).

“Sio kwamba serikali haijachukua hatua wapo wengine ni mabinti zetu,ndugu zetu ambao ukaa vijiweni na kubahatisha ili wapate pesa, lakini ili kukomesha tabia hiyo tutawaweka wazi  wajulikane kwa kufuata kanuni,taratibu na sheria.

“Mimi mwenyewe hizo meseji nimetumiwa na mtu, anasema nitume pesa anifanyie maombi, sasa ili mikakati ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa Watanzania kufikia ulimwengu wa kidigitali ni lazima tukomeshe na kutokomeza mtandao huo,” amesema.

Mahundi ameagiza sekta binafsi kuweka nguvu kubwa kuhakikisha maeneo yenye changamoto za mawasiliano kufikiwa.

“Jamani ongezeni matumizi ya teknolojia za kidigitali kwa kusaidia wananchi matumizi sahihi na utunzaji wa namba za siri  sambamba na kutoa elimu kwa watoa huduma wakiwepo wasajili laini ili kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza,” amesema.

Pia, ameagiza wadau wa sekta binafsi nchini kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa kwa wakuu wa wilaya, viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na wabunge pindi wanapokwenda kufanya tafiti mbalimbali za kuboresha mawasiliano.

Mkuu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mhandisi Richard Sotery amesema kuna miradi mbalimbali walipata ruzuku inaendelea kitekelezwa katika baadhi ya vijiji kikiwepo cha Chilulumo.

Mkazi wa Mji wa Tunduma, Ethelaus Lusungu amesema kumekuwepo na changamoto ya mwingiliano wa mawasilino ya simu katika baadhi ya maeneo mpakani hususani kwa nyakati za usiku na kuomba serikali kuliona hilo ili kulinda usalama.

Related Posts