Sh1.8 bilioni kujenga kiwanda cha kuchakata pamba Mwanza

Mwanza. Chama Kikuu cha Ushirika Nyanza (NCU 1984) kimeanza mchakato wa kujenga kiwanda cha kuchakata pamba kitakachogharimu zaidi ya Sh1.8 bilioni.

Akizungumza leo Ijumaa Machi 21, 2025 wakati wa mkutano mkuu wa 33 wa chama hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya NCU 1984, Leonard Jabalima amesema kiwanda hicho kitakuwa eneo la Manawa, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza.

Katika mkutano huo uliotoa nafasi kwa wajumbe wa vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) 245 kujadili utekelezaji wa shuguli za chama hicho kwa mwaka uliopita, Jabalima amesema Kampuni ya Bajaji Steel kutoka India ndiyo itajenga na kukikamilisha kiwanda hicho.

“Taratibu za awali tayari tumezikamilisha na tumekubaliana malipo ya Dola za Kimarekani 700,000 kwa fedha za kitanzania ni kama Sh1.8 bilioni na namna ya kulipa malipo kwa awamu tumeshakubaliana.

“Kwa hiyo, kikubwa tulichokuwa tunasubiri ni kwenda Dodoma kwa Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuwapa taarifa zote lakini pia kuzungumza na watu wa hazina kukubaliana namna ya umiliki kwa kuwa kiwanda cha Manawa kina umiliki kati ya Nyanza na Serikali,” amesema.

Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika mkoani Mwanza, Hilda Boniface akizungumza na wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mwanza cha Nyanza (NCU 1984) katika mkutano mkuu wa 33 wa chama hicho.

Amesema kiwanda hicho kitakapoanza kufanya kazi kitafungua fursa nyingi ikiwemo wakulima kuuza pamba kwa bei nzuri pamoja na uhakika wa sehemu ya kuuza zao hilo.

“Lakini jambo lingine Amcos zetu zitaimarika na kuanza kufanya kazi moja kwa moja na chama kuliko ambavyo zinafanya kwa sasa kwa kutumia wafanyabiashara binafsi,” ameongeza.

Amesema hata kupata mikopo itakuwa rahisi kwa vile taasisi za kifedha zinasisitiza chama hicho kuwa na kiwanda ili kutoa fedha zitakazonunua malighafi ili kiwanda kichakate na kuongeza thamani.

Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Mwanza, Hilda Boniface amesema lengo la ujenzi wa kiwanda hicho ni kuongeza thamani ya zao la pamba kwa wanaushirika wanaolima zao hilo mkoani Mwanza na nje ya mkoa huo.

“Unapoongeza thamani ya mazao unasababisha bei kuongezeka, unapoongeza thamani ya mazao unasababisha watu kupata morali ya kuongeza uzalishaji…kama tunavyofahamu kwa muda mrefu bei ya pamba imekuwa ikicheza, inashuka na kupanda kwa namna fulani, hii inatokana na kuuza pamba ghafi,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Wakulima watanufaika kwa sababu kutakuwa na bei ya awali ya kununua pamba lakini baada ya kuchakata na kuuza nje ya nchi au kuuza kwa wanunuzi wakubwa watapata tofauti ya bei na wanaweza kurudisha malipo ya pili kwa wakulima.”

Amesema wana imani Nyanza ikichakata pamba, mkulima atanufaika kwa kupata bei bora na malipo ya pili ambayo ni nyongeza ya malipo baada ya pamba kuchakatwa.

Mkulima wa pamba, Rahel Mashenji amesema kiwanda hicho kikikamilika wakulima watanufaika kwa kuwa watauza pamba kwa bei nzuri akieleza msimu uliopita waliuza kilo moja ya pamba Sh1,050, fedha ambayo hailingani na gharama za kilimo hicho.

“Kulima pamba ni gharama…maana kunakupanda, parizi, kuvuna, ukate kate miti uchome…kuna gharama. Tunaomba safari hii bei ya pamba iongezeke, wakulima ndio watapata nguvu ya kufanya kazi,” amesema.

Awali, akifungua mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amevionya vyama vya msingi kutojihusisha na ubadhirifu wa mali za wanachama akisema Serikali ipo macho inavifuatilia.

Amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ili kuhakikisha ustawi wa vyama hivyo na kusimamia kwa ukaribu shughuli za ushirika.

“Katika mkoa wetu, mrajisi hajaniambia vyama ambavyo vina ufisadi ndani yake au Amcos lakini endapo ataniletea taarifa kwamba kuna ufisadi, wizi, kuna uongozi mbovu wa chama fulani au Amcos Fulani, hatutosita kuchukua hatua,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Mara nyingi ninyi wana ushirika mnasema ushirika auingiliwi lakini Serikali ndiyo ilianzisha ushirika na lazima tufuatilie kwa sababu ushirika upo kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na Watanzania siyo kwa ajili ya maendeleo ya viongozi wa ushirika.”

Related Posts