Dar es Salaam. Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB Global) imetenga Euro 1.2 milioni (takribani Sh3.5 bilioni) kutoa msaada wa kiufundi kwa miji ya Afrika Mashariki, kwa maandalizi ya miradi ya miji endelevu inayostahimili mabadiliko ya tabianchi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na EIB Machi 20, 2025 maeneo yatakayonufaika ni Zanzibar nchini Tanzania, Kericho, Nyamira, Kisumu, Embu, Eldoret na Malindi nchini Kenya na Makindye, nchini Uganda.
Makamu wa Rais wa EIB, Thomas Ostros amesema: “Miji na serikali za mitaa zinashikilia jukumu muhimu katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa sababu zinakutana na athari zake kwa kiwango kikubwa.”

Hata hivyo, amesema miji inapata changamoto za miundombinu inayoshindwa kustahimili athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa kukosa rasilimali na utaalamu wa kuunda miradi imara inayoweza kuhimili na kuvutia uwekezaji.
“Kupitia kwa Gap Fund, EIB inasaidia miji kufikia ufumbuzi wa changamoto hizi na kuandaa miradi madhubuti ya kukabili mabadiliko ya tabianchi.”
Taarifa ya EIB imesema katika mambo yatakayofanyika ni tathmini ya chaguzi za usimamizi wa taka ngumu na majitaka, nishati kutoka kwa taka kupitia uzalishaji wa biogasi na matibabu ya majitaka.
“Suluhisho zilizopendekezwa awali zinajumuisha mipango ya usimamizi wa taka ngumu, inayohusisha utenganishaji wa taka kwenye chanzo, urejelezaji wa taka na utupaji wa taka kwa njia inayofaa,” imesema sehemu ya ripoti hiyo.
Pia msaada wa kiufundi kutafuta suluhu ya usafiri usiotegemea vyombo vya moto vinavyotumia nishati chafu, kupunguza athari za mafuriko na kuimarisha uendelevu wa kimazingira kwa kuanzisha maeneo ya wazi ya kupumzika, misitu ya mijini na bioanuai.

Kwa Zanzibar, msaada unalenga kufanya uchambuzi wa kutibu majitaka na kutoa mapendekezo na machaguo bora, kujenga uwezo na kuandaa mpango wa utekelezaji.
Meneo ya mijini yana mchango mkubwa katika mustakabali wa mabadiliko ya tabianchi, kwani zaidi ya nusu ya watu duniani wanaishi katika miji ambayo inachangia asilimia 80 ya uchumi na asilimia 70 ya utoaji wa hewa ya ukaa.
Ukuaji wa miji isiyopangwa huongeza hatari za mabadiliko ya tabianchi, licha ya juhudi za kuunda miji yenye uzalishaji mdogo wa kaboni. Hata hivyo, changamoto za upatikanaji wa fedha na upangaji miradi zinakwamisha utekelezaji wake.
Mfuko wa City Climate Finance Gap Fund unatoa msaada wa kifedha na kiufundi kwa miji ya nchi za kipato cha chini na cha kati, kusaidia kubuni miradi endelevu na kupata fedha za tabianchi.
Tangu mwaka 2020, Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) imesaidia miji 137 kupitia mfuko huu.