Sheria maalumu kukabili changamoto za wazee

Morogoro. Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Mkoa wa Dar es Salaam, Salim Matimbwa amesema changamoto za jumla zinazowakabili wazee zinatokana na kukosekana kwa sheria maalumu itakayosimamia ustawi wa wazee.

Matimbwa ameyasema hayo mkoani Morogoro kwenye mafunzo yaliyoandaliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la HelpAge kwa lengo la kuelimisha wazee namna ya kujua haki na wajibu wao, sheria za mirathi na namna ya kutunza afya zao.

Mabaraza 11 kutoka mikoa na halmashauri mbalimbali nchini yameshiriki mafunzo hayo huku ikibainishwa kwamba matukio ya ukatili dhidi ya wazee yamepungua ukilinganisha na miaka ya nyuma.

“Wazee wa nchi hii hawana sheria inayosimamia haki zao, iliyopo sasa ni sera tu, na hata haya mabaraza ya wazee yaliyopo wapo baadhi ya wakurugenzi, makatibu tawala wa wilaya na mikoa hawayatambui.

“Ifike mahala itungwe Sheria inayowahusu wazee, kuna wazee hasa wa vijijini wanakabiliwa na changamoto nyingi za kiafya na ukatili ikiwemo kuuawa kutokana na migogoro ya ardhi,” amesema Matimbwa.

Kwa upande wake, Leah Nzali, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Wilaya ya Kilosa amesema wazee wa kike wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kuachiwa wajukuu kulea huku wazazi wa watoto hao wakikimbilia mijini kufanya starehe.

“Sisi mabibi tunateseka na malezi ya wajukuu, kijana au binti akishazaa huko mjini anakuja kukubwagia watoto kijijini na baya zaidi hawakumbuki kuleta fedha za matumizi ya watoto wao, bibi unahangaika kufanya kazi ya vibarua ili ulishe wajukuu.

“Wengine ndiyo hata kuja kuwaona watoto hawaji na ikitokea wanatuma fedha basi haizidi Sh20,000 na hiyo ni baada ya miezi sita kupita,” amesema Nzali.

Ameongeza kuwa: “Mimi nimeshawaambia wanangu sina muda wa kulea wajukuu, wakija waje kutembea na waondoke kwa sababu nikisharuhusu wajukuu pale nyumbani, nitakosa muda wa kupumzika, uzee ni pamoja na kupumzika na kuishi sehemu yenye utulivu, makelele ya wajukuu yatakuja kunipa kisukari na presha bure, kila mtu alee mtoto wake mwenyewe.”

Mwenyekiti wa Bazara la Wazee wa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Laurent Mihayo amesema matukio ya mauaji ya wazee (vikongwe) katika mkoa huo yanayotokana na imani ya kishirikina, yamepungua kwa zaidi ya asilimia 90 tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Mihayo amesema kwa sasa matukio ya mauaji yaliyobaki ni yale yanayohusisha migogoro ya mashamba ndani ya familia ama koo kwa koo pamoja na mirathi hasa inayohusu mali kama mashamba na nyumba.

Hata hivyo, amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali yakiwemo mashirika, imekuwa ikiendelea kupiga vita na kuchukua hatua za kukomesha mauaji ya aina hiyo.

Akieleza changamoto nyingine zinazowakabili wazee na vikongwe wa mkoani Shinyanga, Mihayo amesema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za kiafya, kiuchumi, ulinzi na usalama na ushirikishwaji kwenye mambo ya kitaifa.

Akitoa taarifa ya mafunzo hayo, meneja mradi wa shirika lisilo la kiserikali la HelpAge, Joseph Mbasha amesema mafunzo hayo yamelenga kuwafundisha wazeee kujua wajibu na haki zao kuanzia ngazi ya jamii na kuona namna ya kuzitatua changamoto zao.

Mbasha amesema kupitia mafunzo hayo, wameweza kujadili sera mbalimbali zinazohusu wazee ikiwemo Sera ya Wazee ya mwaka 2003 na Sera ya Afya ya mwaka 2007 na kwamba kupitia watoa mada ambao ni wanasheria kutoka Kituo cha Msaada wa Kisheria cha Paralegal, wamewafundisha wazee hao Sheria ya Mirathi na Umiliki wa Ardhi.

Related Posts