Na Oscar Assenga, TANGA.
MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira ( Tanga Uwasa) imebuni mbinu mpya za kukabiliana na maji yanayopotea kila siku ambao utakuwa chachu ya kuwarahisishia kupata taarifa kwa wakati na kufikia kwa haraka kuitatua .
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa Usambazaji wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Mamlaka hiyo Mhandisi Salum Hamis wakati wa kikao cha wadau wiki ya Maji 2025 kilichofanyika leo Jijini Tanga .
Katika kikao hicho mada mbalimbali zilijadiliwa ikiwemo hali ya huduma,mapitio ya mkataba wa huduma kwa wateja na udhibiti wa maji yanayopotea.
Ambapo katika kukabiliana nalo wameandaa mfumo huo ambao utakuwa ukitumika kwa wale wenye simu janga utawasaidia popote wanatapokuwa wakiingia kwenye mfumo wanapiga picha eneo lenye mvujo na kuingia kwenye mfumo na kuandika mvujo.
Alisema baada ya kuandika kupitia mfumo huo utaonekana ukiwa umeripotiwa muda gani na kama umechelewa kufanyiwa kazi itaonekana na kuwarahisishia wao kama wanataka kutoa adhabu kwa watendaji wazembe kuwachukulia hatua watajua kutokana na mfumo kuwaonyesha.
“Mpaka sasa kuna kiasi kikubwa cha maji yanayopotea na tuna zaidi ya asilimia 30 ya maji wanayozalisha kwa mwezi yanapotea hii maana yake ni pesa maana hayo maji tunakuwa tayari tumeyagharamia kwa upande wa kuyawekea dawa na umeme”Alisema
“Kwetu hili ni hasara kubwa sana na ndio maana wanathamini Taarifa za mivujo ya maji tukifanikiwa wa kupunguza maji yanayopotea hata kwetu gharama za uendeshaji zitapungua kwa kiasi kikubwa”Alisema Mhandisi Hamisi.
Katika hilo tumejipanga pia kuongeza vitendea kazi kwa watumishi ikiwemo kugawa pikipiki kuwasambaza zaidi kuhakikisha kila eneo kunakuwa na watu wao ikiwemo magari au pikipiki na bajaji ili kuhakikisha wanakabiliana na upotevu huo kwa hali na mali
“Lakini niwaambie kwamba mfumo huo utawasaidia wadau, wananchi kuweza kuripoti taarifa zao za mivujo na hivyo kuwa rahisi kuweza kufanyiwa kazi na mtu aliyekabidhiwa eneo lake la utendaji kazi na namna anavyo hudumia wateja na kama hawajibiki mfumo utawaonyesha na kuona namna ya kumchukulia hatua”Alisema
Awali akizungumza wakati akifungua kikao hicho Kaimu Mkurugenzi wa Tanga Uwasa Victor Mollel amewataka wadau kuendelea kuwapatia taarifa za changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo kwa sababu zinawasaidia katika kuboresha taarifa zao za utendaji wa kazi.
Alisema kauli mbiu ya mwaka huu ya maji ni uhifadhi uoto asili kwa uhakika wa maji wao wanajua chanzo cha maji cha Jiji la Tanga yanatoka Amani Muheza kwenye Mto Zigi hivyo kuna jitihada mbalimbali yanaendelea kwa ajili ya uhifadhi wa Mazingira.
Naye kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Huduma kwa Wateja Daudi Mkumbo alisema katika mkataba au rasimu ya mkataba mpya ya huduma kwa mteja Tanga Uwasa inaowajibu wa kutowakatia wateja huduma ya maji kwa siku za mapumziko kama Jumamosi, Jumapili na Ijumaa kuaza saa sita mchana
Mkumbo ambaye pia ni Meneja wa Huduma kwa Wateja alisema hiyo inatokana na kwamba katika wakati huo wakazi wa Tanga wengi wapo kwenye ibada hiyo itawawia vigumu katika kushughulia kurudisha maji, siku za mapumziko wahudumu wakiwemo mafundi kuwa kwenye mapumziko.