Tatizo la afya ya akili linavyotesa wafanyakazi maeneo ya kazi

Wakati takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zikionesha kwenye kila wafanyakazi wa tano mmoja ana msongo wa mawazo utokanao na kazi, wadau wa afya ya akili wameonesha namna msongo huo unavyotesa wafanyakazi ofisini na kusababisha tatizo la afya ya akili.

Kwa mujibu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ya mwaka 2023 iliyolenga kuangalia hali ya afya ya akili kwa mwaka 2020, hali hiyo imechangia asilimia 8.15 ya vifo vya kujinyonga kwa kila watu 100,000.

Kwa upande wake, ripoti ya Wizara ya Afya ilieleza kuwa tatizo la maradhi ya afya ya akili, limepanda kutoka wagonjwa 386,358 mwaka 2012 hadi 2,102,726 kufikia mwaka 2021, likiwa ni ongezeko la asilimia 82.

Mtaalamu wa afya ya akili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora Kitete, ambaye pia ni Mratibu wa afya ya akili mkoani humo, Dk Swaumu Kimaro anasema wafanyakazi wengi wanakumbwa na tatizo hilo, kwa kutokubali kulisema kwa wengine, matokeo yake ni kusababisha magonjwa yasiyoambukiza, hasa presha, kisukari na kushuka kwa kinga ya mwili.

“Wafanyakazi wengi kweli tunateseka na hizo changamoto za afya ya akili na hizi changamoto kwa wafanyakazi zinawatesa kwa sababu wengi tunakuwa na unyanyapaa juu ya afya ya akili, mtu anateseka na stress zake (msongo) anashindwa kufunguka anabaki nao, mwisho wa siku anakuja kupata magonjwa ya ndani kama presha, kisukari, kinga ya mwili kushuka na wakati mwingine kwa sababu ya msongo wa mawazo, mapigo ya moyo yanakwenda mbio,” anasema.

Anasema mfanyakazi anahitaji kujua namna ya kuzuia changamoto hiyo, lakini kwanza ni lazima ajue dalili ambazo zinaweza kumuonesha kama ameathiriwa na tatizo hilo, ikiwemo ya kutokuwa na hamu ya kufanya kazi au kufanya kazi kupitiliza, mfadhaiko, kupoteza matumaini, kuwa na hasira kila wakati na wasiwasi uliopitiliza.

“Ikiwa unajikuta tu umepata hasira za hapa na pale, unajikuta saa nyingine unalia mwenyewe, unajikuta usingizi hupati usiku, unakuwa na vitabia fulani… saa nyingine unajikuta unakula sana, saa nyingine huli sana. Unajitenga na wenzako, kwa hiyo ukishaziona hizo dalili inabidi umuone mtaalamu wa afya ya akili mapema kabla hali haijawa mbaya,” anasema Dk Kimaro.

Anasema kuna matibabu ya aina mbili hadi tatu kulingana na jinsi ambavyo mtu amepata changamoto hiyo, ikiwemo matibabu kwa njia ya dawa, kwa njia ya mazungumzo ambayo yanasaidia mtu kupona haraka changamoto aliyonayo.

“Cha msingi, tujifunze kupotezea…mtu unapopata janga au matatizo ujifunze kukabiliana na msongo wa mawazo kwamba hili tatizo limetokea, ni la kwangu… Ukiendelea kulibeba ndio unazidi kuumia, sisi binadamu hatuwezi kuzikwepa jitahidi kufanya mazoezi asubuhi na jioni na kulala mapema,” anaongeza.

Akizungumzia namna afya ya akili inavyowatesa wafanyakazi, Mkurugenzi wa Shirika la Akili Platform Tanzania linalohusika na afya ya akili, mazingira na haki za binadamu, Roghat Robert anasema changamoto hiyo siyo tu inaweza kumfanya mtu kuwa mpweke, lakini pia anaweza kujiua.

Anasema kuna sababu mbalimbali zinazochangia wafanyakazi kuwa na ugonjwa huo, zikiwamo mgogoro mahala pa kazi, maslahi au ujira mdogo kulinganisha na kazi anazozifanya, kufikiria usalama wa kazi unaomfanya mara kwa mara afikirie kufukuzwa hata kama hajaambiwa.

“Unakuta eneo la kazi hakuna mapatano..bosi anafokea wafanyakazi, wafanyakazi wanakoromeana wao kwa wao, majungu yanakuwa ni mengi, kazi za muda mrefu, majukumu mengi wakati mwingine kupita uwezo wa mfanyakazi anachokipata…” anasema na kuongeza:

“Kwa hiyo, unakuta huyu mfanyakazi malengo yote anakuwa ameyaweka ili akamilishe kazi ya bosi na mshahara uweze kuingia. Kufanya kazi kupitiliza napo kunaweza kumsababishia mfanyakazi kupata matatizo ya afya ya akili.”

Anasema kingine kinachosababisha tatizo hilo ni wafanyakazi wengi hawatambui wajibu wao katika kudai haki zao, hivyo usalama wa kazi zao na maisha yao huwa unakuwa ni mdogo, akieleza kama mtu anafanya kazi katika mazingira hayo, lazima atafanya kazi kwa kwa presha kubwa na wakati mwingine bila utulivu.

Pia anataja mabadiliko ya nafasi ya mara kwa mara kazini yanaweza kusababisha matatizo hayo, akitolea mfano kupunguza wafanyakazi au kuwaondoa kwenye nafasi zao, kunawafanya wanaobaki kuwaza muda wowote nao wataondolewa, hivyo kuwa na msongo wa mawazo unaoweza kusababisha matatizo ya afya ya akili.

“Uhusiano mbaya kati ya bosi na mwajiriwa, mfano mtu anakuwa anafanya kazi akipatia vizuri hapongezwi, ila akikosea tu tayari ndio palepale wanapodakia, nilijua tu utakosea..nilijua tu utachelewa, yaani haangalii kwa nini huyu mtu amekosea anakuwa tayari na majibu yake,” anasema.

Anaongeza pia majungu kazini na baadhi ya watu wanaofikisha kila taarifa au tukio linalofanyika ofisini kwa bosi, inaathiri akili za wafanyakazi, hasa wanaonyanyapaliwa au kutengwa, akiwataka waajiri watambue umuhimu wa kujali afya ya akili ya waajiriwa wao.

Namna ya kukabiliana na msongo wa mawazo kazini

Akizungumzia namna ya kukabiliana na tatizo hilo kazini, mwanasaikolojia na mnasihi, Jesusa Malewo anasema hakuna njia za moja kwa moja kuzuia matatizo ya afya ya akili, bali, mfanyakazi afahamu anachopitia kisha kuwa mvumilivu, mstahimilivu, kufanya jitihada binafsi kukabiliana na msongo, lakini pia kukubaliana na ukweli.

“Kama watu watajijengea kuwa wastahimilivu itawasaidia kuondokana na changamoto kazini na wanaweza kuwa wastahimilivu kwa kujifunza, kuangalia je, kuna kitu gani naweza kufanya kutatua tatizo, lakini pia kuangalia njia mbalimbali za kutatua tatizo kwa muda huo,

Anasema wafanyakazi wanapopata changamoto za afya ya akili wanapaswa kuwashirikisha watu wanaowaamini kwamba watawasaidia. Pia kujenga tabia ya kutafuta msaada wa kisaikolojia kwa kuwa wanasaikolojia wanaweza kumjengea mwathirika ujuzi mbalimbali ambao unaweza kumsaidia aweze kuendana na kile kinachomkabili.

Anasema wafanyakazi wengi wakipata matatizo wanatumia pombe kama njia pekee ya kusuluhisha matatizo yao, kitu ambacho siyo sawa, akini pia wanafanya matumizi makubwa ya vitu, akitolea mfano kula sana na kujiingiza kwenye vitu anavyoamini vitatatua tatizo, kumbe siyo.

“Watu wanapaswa kuwa makini na mtindo wa maisha pale wanapopitia changamoto za afya ya akili. Mfano kuna watu wanatumia mitandao ya kijamii, kuna watu wengine hawalali kwa sababu tu wanapitia matatizo au changamoto…kwa hiyo wasipolala ile changamoto inazidi kuongezeka,” anasema.

Anaongeza kuwa njia nyingine ya kukabiliana na tatizo hilo ni wafanyakazi wajifunze kukabiliana na msongo wa mawazo, akieleza binadamu ameumbiwa kupitia msongo, hivyo lazima atafute njia ya kutatua matatizo pamoja na kujifunza kutawala hisia zake.

Naye, mfanyakazi wa moja ya taasisi za kifedha jijini Mwanza, Queen Mangu anasema waajiri wana nafasi kubwa ya kuwaepusha waajiriwa wao na msongo wa mawazo unaoweza kuwasababishia wasiwasi wa nafasi zao kazini, ambao ndio chanzo cha matatizo ya afya ya akili kwa kuzungumza nao kwa upole wanapokosea, lakini pia wazingatie malipo mazuri ya ujira wao.

Related Posts