MAMLAKA ya Mapato Tanzania imetangaza majina 112,952 ya waliokidhi vigezo vilivyowekwa na hivyo kuitwa kwenye usaili wa mchujo wa kuandika huku idadi ya wanaotakiwa kuajiriwa kutoka kada mbalimbali ikiwa ni 1,596.
Mapema mwezi Februari mwaka huu,, Kamishna Mkuu wa TRA Yusuph Mwenda akiwa Dodoma alisema wamepokea maombi ya watu 135,027 katika nafasi za ajira zilizotangazwa na Mamlaka.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Mamlaka hiyo leo Machi 21, 2925 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Mkurungenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na utawala wa TRA, Moshi Kabengwe amesema katika mchakato huo Mamlaka imezingatia taratibu zote za kupata waajiriwa kupitia usaili.
“TRA imepitia kwa umakini mkubwa maombi yote yaliyopokelewa na kupata waomba kazi 112,952 waliokidhi vigezo vilivyowekwa na hivyo kustahili kuitwa kwenye usaili wa mchujo wa kuandika (written interview) ambao unatarajiwa kufanyika kuanzia Machi 29 hadi 30 mwaka huu.” Amesema Kabengwe.
Amesema kuwa majina ya waliofanikiwa yatatangazwa kwenye tovuti ya TRA (www.tra.go.tz) kuanzia leo machi 22,2025 na pia taarifa zitatumwa moja kwa moja kwa kila muombaji kupitia barua pepe yake aliyotumia wakati wa kuomba kazi, vilevile tarehe, mahali na muda wa usaili zimeonyeshwa kwenye wito huo.”
Amesema usaili huo wa mchujo wa kuandika utafanyika katika mikoa tisa ambayo ni Dar es Salaam ikihusisha mkoa huu na Pwani, Zanzibar (Unguja na Pemba) Arusha ambayo itahusisha waombaji kutoka Arusha, Manyara, Kilimanjaro na Tanga.
Mikoa mingine ni Dodoma ambayo itahusisha waombaji kutoka Morogoro, Dodoma, Singida, Iringa na Tabora. Pia mkoani Mtwara ambayo itakuwa na watu kutoka Mtwara, Lindi na Ruvuma huku mkoa wa Mbeya ukihusisha mikoa ya Mbeya, Songwe na Rukwa. Aidha Mwanza itahusisha, Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu wakati ,Kagera ikihusisha Kagera na Geita na Kigoma ambayo itahusisha waombaji kutoka Kigoma na Katavi.
Kabengwe amesema utaratibu maalumu umeandaliwa kwa waombaji kazi wenye mahitaji maalumu ili waweze kufanya usaili huo bila usumbufu.
“Mchakato huu utaendeshwa na mshauri Mtaalamu (Consultant) na Mamlaka itasimamia kwa karibu ili kuhakikisha haki inatendeka kwa waombaji wote. Aidha tunatoa wito kwa waombaji kazi wote kujiandaa vyema katika hatua zote za usaili ili kufanya vizuri katika mitihani hiyo na kuepuka udanyanyifu wa aina yeyote,”amesema Kibengwe.
Amesema, waombaji watakaofaulu kwenye usaili wa mchujo wa kuandika wataitwa kwenye usaili wa mahijiano kwa tarehe, siku na mahali watakapotaarifiwa baadae.
Mkurungenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Moshi Kabengwe akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Mamlaka hiyo leo Machi 21, 2025 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo wakati akitangaza waombaji kazi 112,952 waliopita katika mchujo wa kwanza kati ya 135,027 waliiomba nafasi za kati katika Mamlaka hiyo.