Tuna waliomaliza kidato cha sita, digrii hawawezi kupika chakula- Dk Biteko

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema ni kawaida kuona mtoto amemaliza kidato cha sita ama digrii ya elimu fulani, lakini hawezi kujipikia chakula chake mwenyewe.

Amesema Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) ina uwezo na jukumu la kubadilisha Tanzania kama jamii itakubaliana watoto kupata stadi fulani kwa ajili ya kuboresha maisha.

Dk Biteko ameyasema hayo leo Ijumaa Machi 21, 2025 wakati akimwakilisha wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Miaka 50 ya Veta iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Aidha, Dk Biteko ameendelea kutilia mkazo mjadala wa elimu ya Veta kwa lengo la kujipatia ujuzi zaidi hata kwa wale wanaomaliza elimu za juu.

Dk Biteko amesema Serikali imeweka msukumo mkubwa katika ufundi stadi ili Watanzania wapate elimu yenye viwango vikubwa na ujuzi wa kuweza kujikomboa katika nyanja za kiuchumi na kijamii.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anajenga Veta kila wilaya ili kuwapa ujuzi Watanzania waweze kuajirika katika sekta zote,” amesisitiza Dk Biteko.

Pia, ameipongeza Veta imepiga hatua kubwa na kuwataka kuendelea kufanya kazi ili kuwajengea uwezo Watanzania katika ujuzi mbalimbali.

Vilevile, amesisitiza elimu kutolewa kwa watu wenye mahitaji maalumu na wanaotoka kwenye mazingira magumu nchini ili iweze kuongeza fursa kwa kila Mtanzania kupata elimu ya ujuzi.

Related Posts