Katika kipindi hiki cha Ramadhani kwa Waislamu na Kwaresima kwa Wakristo, waumini wengi wanatamani kufunga kama sehemu ya ibada yao.
Hata hivyo, kwa wagonjwa wa kisukari, kufunga kunaweza kuwa changamoto kubwa kutokana na athari za mabadiliko ya sukari mwilini.
Mwongozo wa kufunga kwa usalama kwa wagonjwa wa kisukari, unategemea mambo kadhaa muhimu ya kuzingatia.
Kabla ya kuamua kufunga, mgonjwa wa kisukari anapaswa kushauriana na daktari wake. Wagonjwa wa kisukari wanaotumia insulini au dawa kali za kushusha sukari wanaweza kuwa katika hatari kubwa ya sukari kushuka kupita kiasi au sukari kupanda kupita kiasi wakati wa kufunga. Hivyo, ni muhimu kupata ushauri wa kitaalamu.
Kwa baadhi ya wagonjwa, hususan wale wenye udhibiti mzuri wa sukari yao, kufunga kunaweza kuwa salama ikiwa hatua za tahadhari zitachukuliwa.
Lakini kwa wale wenye matatizo sugu kama ugonjwa wa figo au historia ya kushuka sana kwa sukari, kufunga kunaweza kuwa hatari na hivyo kuepukwe.
Ikiwa mgonjwa wa kisukari ataamua kufunga kwa kufuata ushauri wa daktari, hapa kuna mbinu muhimu za kuhakikisha afya yake inasalia salama.
Ni muhimu kupima sukari mwilini mara kwa mara, angalau mara tatu kwa siku, kwa maana ya asubuhi, katikati ya mchana na jioni kabla ya kufuturu.
Ikiwa sukari itashuka chini ya 4 ni muhimu kuvunja mfungo mara moja na kunywa juisi au kula chakula chenye sukari ili kurejesha kiwango cha sukari katika hali ya kawaida.
Wakati ya kufuturu, kwa wagonjwa wa sukari ni muhimu kuanza kwa maji ya moto au maziwa ya moto na siyo kwa maji baridi, kisha kula tende moja au mbili.
Tende zina sukari ya asili inayosaidia kurejesha nguvu haraka bila kusababisha ongezeko kubwa la sukari mwilini.
Epuka vyakula vyenye mafuta mengi au sukari nyingi kama vile vyakula vya kukaanga au vinywaji vyenye sukari nyingi.
Badala yake, chagua vyakula vyenye nyuzinyuzi nyingi kama nafaka nzima, mboga za majani, na vyanzo vya protini kama nyama isiyo na mafuta au samaki.
Epuka kufanya mazoezi magumu. Kufanya mazoezi mazito wakati wa kufunga kunaweza kusababisha kushuka kwa kiwango cha sukari mwilini. Ikiwa unahitaji kufanya mazoezi, yafanye mepesi kama kutembea taratibu jioni kabla ya futari.
Kufunga ni ibada muhimu kwa waumini wa dini mbalimbali, lakini kwa wagonjwa wa kisukari, inahitaji tahadhari kubwa.
Ushauri wa daktari ni jambo la msingi kabla ya kuamua kufunga, na ni muhimu kufuatilia viwango vya sukari mwilini mara kwa mara.
Kwa kufuata mwongozo sahihi, mgonjwa wa kisukari anaweza kushiriki katika mfungo kwa usalama bila kuhatarisha afya yake.