Dar es Salaam. Wakati mataifa yakiadhimisha Siku ya Ushairi Duniani, wadau wa Kiswahili na ushairi nchini wameeleza vikwazo vinavyokwamisha ushairi nchini ikiwa ni pamoja na elimu duni na kudharau fasihi ya Kiswahili.
Siku ya Ushairi Duniani huadhimishwa Machi 21 kila mwaka na siku hii ilianzishwa mwaka 1999 na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kwa lengo la kuenzi tofauti ya lugha kupitia ushairi.
Akizungumza na Mwananchi leo Machi 21, 2025 kuhusu siku hiyo, mtaalamu wa Kiswahili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Profesa Aldin Mutembei amesema ushairi unachukua nafasi kubwa katika nyanja za maisha ya kila siku.
Profesa Mutembei ameeleza kuna vitu ambavyo vinasababisha mashairi yasilete maendeleo katika jamii za sasa kutokana na elimu duni hasa katika matumizi ya teknolojia za kidigitali.
“Kutoongezeka kwa ushairi hapa Tanzania, suala la elimu duni hasa kwa baadhi ya watu, limechangia, pia kudharau fasihi kwa ujumla, hali hii ikiendelea inaweza kufuta kabisa ushairi,” amesema.
Hata hivyo, Profesa Mutembei ameongeza kuwa ushairi ni mpana, upo sehemu mbalimbali hasa kwenye nyimbo, ngonjera na muziki.
“Ushairi una dhana pana, pia, unahusisha upande wa nyimbo, ngojera na hata muziki kama Bongo Fleva,” amesema Profesa Mutembezi.
Mwanazuoni huyo ameongeza kuwa nafasi ya ushairi imeendelea kukua na sasa unapata nafasi kubwa katika maeneo mbalimbali ya jamii, ikiwemo siasa, dini, elimu na burudani.
“Kwa sasa hivi, nafasi ya ushairi ipo sehemu nyingi sana hasa kwenye mambo ya siasa, maeneo ya dini, katika elimu pamoja na burudani, tunaona hasa kwenye burudani mara nyingi ushairi pia unatumika,” amesema Profesa Mutembei.
Kwa upande wake, mtunzi wa mashairi, Nassor Mohamed amesema zipo sababu ambazo mashairi yanakandamizwa na kutokuwa na nguvu kwa sasa.
“Kuna sababu ambazo zinafanya ushairi kwa sasa kukosa nguvu na kukandamizwa, kwanza wenye mamlaka kutoupa nguvu ushairi ipasavyo lakini washairi wenyewe kutojisumbua kutoa elimu bora,” amesema.
Pia, ameeleza changamoto inayoathiri ushairi kutoendelea kwa sababu ya wengi wao kuvamia fani hiyo wakati hawana weledi nao kiasi cha uga wa ushairi na kuwa ni fujo.
Mshairi huyo ameitaka jamii ya Watanzania kutambua umuhimu wa ushairi na kujifunza.
“Ushairi bado una nafasi kubwa Tanzania kutokana na kutumika kwa njia mbalimbali katika jamii. Pia, ni kioo cha jamii kinachotumiwa kuimulika ipasavyo na kuipa nafasi ya kujitambua, kujisahihisha panapostahili na kijifunza,” amesema Mohamed.