Arusha. Wizara ya Viwanda na Biashara imewataka vijana wajasiriamali katika sekta ya kilimo ikiwemo wasindikaji wa mazao mbalimbali kuchangamkia fursa katika soko huru la Afrika.
Pia, wametakiwa kuhakikisha wanapozalisha mazao mbalimbali na kuchakata bidhaa, wazingatie sheria na kanuni ili kukidhi mahitaji ya soko ikiwemo usalama wa chakula.
Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Machi 21, 2025 na Ofisa Biashara Mwandamizi kutoka wizarani, Festo Kapela wakati akizungumza na vijana 60 kutoka halmashauri saba za Mkoa wa Arusha, waliopatiwa mafunzo kupitia programu ya Youth Entrepreneurship for the Future of Food and Agriculture (Yeffa).
Festo ambaye ni mratibu wa dawati la chakula na lishe, amesema vijana hao wakitumia elimu wanayoipata kupitia mradi huo wataweza kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika soko huru la Afrika ambalo linahitaji bidhaa zenye ubora.
“Tuko hapa kusisitiza katika eneo la kuongeza thamani mazo, vijana wengi mmeingia kwenye biashara, ni muhimu kutumia mafunzo haya kuboresha bidhaa na mazao mnayozalisha ili zikidhi mahitaji ya soko, kuna soko huru la Afrika linahitaji bidhaa zenye ubora.
“Tunawaelimisha kuhusu kuongeza virutubisho kwenye mazao, mfuate kanuni na sheria pamoja na matumizi ya teknolojia, tutawasaidia kwa kushirikiana na wadau wengine ili kufikia ubora kwenye uzalishaji wa bidhaa zenu, muweze kushindana katika masoko ya ndani na ya kimataifa,” amesema.
Kuhusu usalama wa chakula, amesema ni suala muhimu hasa katika kulinda afya ya mlaji na kufikia matakwa ya kisheria, kuanzia mnyonyoro mzima wa uzalishaji wa chakula lazima usalama wa chakula lipewe kipaumbele,” amesema ofisa huyo.
Awali, meneja anayesimamia urutubishaji wa vyakula viwandani kutoka Shirika la Global Alliance for Improved Nutrition (Gain), Archard Ngemela amesema kupitia programu ya Yeffa wanawasaidia vijana hao kuboresha kilimo na mifumo ya chakula.
Amesema Gain kwa kushirikiana na Agra na Mastercard Foundation, wanatekeleza programu hiyo ya miaka minne inayotekelezwa katika mikoa 12 ambapo lengo ni kuchagiza juhudi za serikali kuboresha maisha ya mkulima kwa kuongeza thamani ya biashara ya mazao na fursa za ajira kwa vijana na wanawake.
“Gain tunashiriki aktika mradi huu upande wa lishe, tunaangalia usalama wa chakula kuanzia uzalishaji hadi mwisho, teknolojia zinazotumika katika kuongeza urutubishaji wa vyakula iwe viwandani au mashambani,”amesema
“Tunawasaidia vijana wajue taratibu, teknolojia zilizopo katika kuzalisha vyakula vyenye lishe lakini vinavyoendana na viwango ili wapate soko la mazao yao na kuongeza kipato,” amesema.
Mmoja wa wanufaika wa programu hiyo ambaye ni mkulima kijana, Jackline Robert amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo hasa kuzingatia usalama wa chakula na kuwa wamejifunza umuhimu wa uongezaji virutubisho katika makundi manne ambayo hutumika katika milo ambayo ni unga wa mahindi, unga wa ngano, mafuta ya kupikia na chumvi.
“Kwa sababu baadhi ya magonjwa ambayo siyo ya kuambukiza yanasababishwa na kukosekana kwa viutubisho katika vyakula vyetu, tumejifunza njia za usindikaji vyakula na kuongeza virutubisho kwa kuzingatia usalama,” amesema.
Awali akifungua mafunzo hayo, mwakilishi wa Ofisa Elimu Mkoa wa Arusha, Mwalimu Tumsifu Mushi amesema mafunzo hayo yatachochea ajira kwa vijana katika sekta ya kilimo, kuongeza ufanisi wa kuyafikia masoko, kuongeza uzalishaji na utekelezaji wa miongozo mbalimbali.
“Sote tunatambua dunia inakabiliwa na changamoto ya usalama wa chakula na mamilioni ya watu duniani kote wanakabiliwa na njaa, utapiamlo na mabadiliko ya tabianchi yanaathiri uzalishaji wa chakula,” amesema.
“Hii ni hasara kubwa, hivyo tukishirikiana tunaweza kujenga mifumo ya chakula ambayo inahakikisha usalama wa chakula kwa wote, inalinda mazingira na inachangia maendeleo endelevu,” ameongeza.